Mark 3

Yesu Amponya Mtu Mwenye Mkono Uliopooza

1Yesu akaingia tena ndani ya sinagogi na huko palikuwa na mtu mwenye mkono uliopooza. 2Wakawa wanamwangalia waone kama atamponya siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. 3Yesu akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Njoo hapa mbele.”

4Kisha Yesu akawauliza, “Je, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kufanya jema au baya, kuokoa maisha au kuua?” Lakini wao wakanyamaza kimya.

5Yesu akawatazama pande zote kwa hasira, akahuzunika sana kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukapona kabisa! 6Kisha Mafarisayo wakatoka nje, mara wakaanza kufanya shauri la kumwua Yesu wakiwa na kundi la wafuasi wa Herode.

Umati Wa Watu Wamfuata Yesu

7Yesu pamoja na wanafunzi wake wakaondoka huko wakaenda baharini, nao umati mkubwa wa watu kutoka Galilaya ukamfuata. 8Waliposikia mambo yote aliyokuwa akiyafanya, umati mkubwa wa watu ukamjia kutoka Uyahudi, Yerusalemu, Idumaya, Ng'ambo ya Yordani pamoja na wale wa sehemu za karibu na Tiro na Sidoni. 9Kwa sababu ya umati mkubwa wa watu, aliwaambia wanafunzi wake waweke tayari mashua ndogo kwa ajili yake, ili kuwazuia watu kumsonga. 10Kwa kuwa alikuwa amewaponya wagonjwa wengi, wale wenye magonjwa walikuwa wanasukumana ili wapate kumgusa. 11Kila mara pepo wachafu walipomwona, walianguka chini mbele yake na kupiga kelele wakisema, “Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.” 12Lakini aliwaonya wasimseme yeye ni nani.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

13Yesu akapanda mlimani na kuwaita wale aliowataka, nao wakamjia. 14Akawachagua kumi na wawili ambao pia aliwaita mitume, ili wapate kuwa pamoja naye na kuwatuma kwenda kuhubiri 15na kuwa na mamlaka ya kutoa pepo wachafu. 16Hawa ndio wale kumi na wawili aliowachagua: Simoni (ambaye alimwita Petro), 17Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye (ambao aliwaita Boanerge, maana yake Wana wa Ngurumo), 18Andrea, Filipo, Bartholomayo, Mathayo, Tomasi, Yakobo, mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkananayo na 19Yuda Iskariote, ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Yesu Na Beelzebuli

20Ndipo Yesu aliporudi nyumbani, umati wa watu ukakusanyika tena, kiasi kwamba yeye na wanafunzi wake hawakuweza kula chakula. 21Ndugu zake walipopata habari wakaja ili kumchukua kwa maana watu walikuwa wakisema, “Amerukwa na akili.”

22Walimu wa sheria waliotelemka kutoka Yerusalemu walisema, “Amepagawa na Beelzebuli
3:22 Beelzebuli kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu
! Kwa kutumia mkuu wa pepo wachafu, anatoa pepo wachafu.”

23Basi Yesu akawaita na kuzungumza nao kwa mifano akasema: “Shetani awezaje kumtoa Shetani? 24Kama ufalme ukigawanyika wenyewe kwa wenyewe, ufalme huo hauwezi kusimama. 25Nayo nyumba kama ikigawanyika yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haiwezi kusimama. 26Naye Shetani kama akijipinga mwenyewe akiwa amegawanyika, hawezi kusimama bali mwisho wake umewadia. 27Hakuna mtu ye yote awezaye kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu, ndipo awezapo kuteka nyara. 28Amin, amin nawaambia, dhambi zote na makufuru yote ya wanadamu watasamehewa. 29Lakini ye yote anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa kamwe, atakuwa na hatia ya dhambi ya milele.”

30Yesu alisema hivi kwa sababu walikuwa wanasema, “Ana pepo mchafu.”

Mama Na Ndugu Zake Yesu

31Kisha wakaja ndugu zake Yesu pamoja na mama yake. Wakiwa wamesimama nje, wakamtuma mtu kumwita. 32Umati wa watu ulikuwa umeketi kumzunguka wakamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.”

33Akawauliza, “Mama yangu na ndugu zangu ni nani?”

34Kisha akawatazama wale watu waliokuwa wameketi kumzunguka pande zote, akasema, “Hawa ndio mama zangu na ndugu zangu. 35Mtu ye yote anayetenda mapenzi ya Mungu huyo ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

Copyright information for Neno