Mark 5

Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo

1Wakafika upande wa pili wa bahari wakaingia katika nchi ya Wagerasi. 2Yesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini akakutana naye. 3Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo, 4kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa kwa minyororo mikononi na miguuni, akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu ye yote aliyekuwa na nguvu za kumzuia. 5Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.

6Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia akapiga magoti mbele yake. 7Akapiga kelele kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!” 8Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”

9Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?”

Akamjibu, “Jina langu ni Legioni
5.9 Legioni maana yake ni Jeshi
, kwa kuwa tuko wengi.”
10Akamwomba sana Yesu asiwapeleke nje ya nchi ile.

11Kundi kubwa la nguruwe lilikuwa karibu likilisha kando ya kilima. 12Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe, turuhusu tuwaingie.” 13Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao 2,000, likatelemkia gengeni kwa kasi nalo likazama baharini.

14Wale waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakatoka kwenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia. 15Walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu Legioni, akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na pia akiwa na akili zake timamu. Wakaogopa. 16Wale walioyaona mambo haya wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule aliyekuwa na pepo wachafu na lile kundi la nguruwe. 17Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.

18Yesu alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Yesu waende pamoja. 19Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana na jinsi alivyokuhurumia.” 20Yule mtu akaenda zake akaanza kutangaza katika Dekapoli jinsi Yesu alivyomtendea, nao watu wote wakastaajabu.

Mwanamke Aponywa

21Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ng'ambo, umati mkubwa wa watu ukamzunguka, yeye akiwa kando ya bahari. 22Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo, akafika pale, naye alipomwona Yesu akapiga magoti miguuni pake, 23akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona.” 24Hivyo Yesu akaenda pamoja naye.

Umati mkubwa wa watu ukamfuata, watu wakawa wanamsonga.
25Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. 26Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi na kutumia kila kitu alichokuwa nacho lakini badala ya kupona hali yake ilizidi kuwa mbaya. 27Alikuwa amesikia habari za Yesu naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake, 28kwa maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi lake tu, nitapona.” 29Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.

30Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akaugeukia ule umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyenigusa?”

31Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi umati wa watu unavyokusonga, wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”

32Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa. 33Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. 34Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

Yesu Amfufua Binti Yairo

35Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”

36Kwa kusikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”

37Hakumruhusu mtu mwingine ye yote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana nduguye Yakobo. 38Walipofika nyumbani kwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa. 39Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa bali amelala tu.” 40Wale watu wakamcheka kwa dharau.

Lakini yeye akawatoa wote nje, akawachukua baba na mama wa yule mtoto pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao. Wakaingia ndani mpaka pale alipokuwa yule mtoto.
41Akamshika mtoto mkono akamwambia, “Talitha koum
5.41 Talitha koum ni lugha ya Kiaramu
!” (Maana yake, “Msichana, ninakuambia, amka!”)
42Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili). Walipoona haya, wakastaajabu sana. 43Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu ye yote jambo hili, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.

Copyright information for Neno