Matthew 1

Kumbukumbu Za Ukoo Wa Yesu Kristo

1Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:

2Abrahamu akamzaa Isaki,
  • Isaki akamzaa Yakobo,
  • Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake,
3Yuda akamzaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari, Peresi akamzaa Hesroni, Hesroni akamzaa Aramu, 4Aramu akamzaa Aminadabu, Aminadabu akamzaa Nashoni, Nashoni akamzaa Salmoni, 5Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu, Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu, Obedi akamzaa Yese, 6Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme. Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria. 7
  • Solomoni akamzaa Rehoboamu,
  • Rehoboamu akamzaa Abiya,
  • Abiya akamzaa Asa,
8Asa akamzaa Yehoshafati, Yehoshafati akamzaa Yoramu 1.8 Yoramu ndiye Yehoramu, maana yake ni Yehova yu juu , Yoramu akamzaa Uzia, 9Uzia akamzaa Yothamu, Yothamu akamzaa Ahazi, Ahazi akamzaa Hezekia, 10Hezekia akamzaa Manase, Manase akamzaa Amoni, Amoni akamzaa Yosia, 11wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake. 12Baada ya uhamisho wa Babeli:
  • Yekonia alimzaa Shealtieli,
  • Shealtieli akamzaa Zerubabeli,
13Zerubabeli akamzaa Abiudi, Abiudi akamzaa Eliakimu, Eliyakimu akamzaa Azori, 14Azori akamzaa Zadoki, Zadoki akamzaa Akimu, Akimu akamzaa Eliudi, 15Eliudi akamzaa Eleazari, Eleazari akamzaa Matani, Matani akamzaa Yakobo, 16naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo 1.16 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Mpakwa (au Aliyetiwa) mafuta . 17Hivyo, kulikuwapo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.

Kuzaliwa Kwa Yesu Kristo

18Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

20Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu
1:21 Yesu ni Kiyunani, kwa Kiebrania ni Yoshua au Yeshua, maana yake ni Yehova ni wokovu
, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.”

22Haya yote yametukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23“Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli,” maana yake, “Mungu pamoja nasi.”

24Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake. 25Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.

Copyright information for Neno