Matthew 10

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

Ndipo Yesu akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa mamlaka juu ya pepo wachafu kuwatoa na kuponya kila ugonjwa na maradhi ya kila aina.

Haya ndiyo majina ya hao wanafunzi kumi na wawili: wa kwanza, Simoni, aitwaye Petro na Andrea nduguye, Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana nduguye, Filipo na Bartholomayo, Tomasi na Mathayo mtoza ushuru, Yakobo mwana wa Alfayo na Thadayo, Simoni Mkananayo na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu.

Hawa kumi na wawili, Yesu aliwatuma akawaagiza, “Msiende miongoni mwa watu Mataifa wala msiingie mji wo wote wa Wasamaria. Lakini afadhali mshike njia kuwaendea kondoo wa nyumba ya Israeli waliopotea. Wakati mnapokwenda, hubirini mkisema, ‘Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’ Ponyeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo wachafu. Mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala shaba kwenye vifuko vyenu. 10 Msichukue mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala jozi ya pili ya viatu, wala fimbo, kwa maana mtenda kazi anastahili posho yake.

11 “Mji wo wote au kijiji cho chote mtakapoingia, tafuteni humo mtu anayestahili, nanyi kaeni kwake mpaka mtakapoondoka. 12 Mkiingia kwenye nyumba, itakieni amani. 13 Kama nyumba hiyo inastahili, amani yenu na iwe juu yake, la sivyo, amani yenu na iwarudie ninyi. 14 Kama mtu ye yote hatawakaribisha ninyi, wala kusikiliza maneno yenu, kung'uteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu mtakapokuwa mnatoka kwenye nyumba hiyo au mji huo. 15 Amin, amin nawaambia, miji ya Sodoma na Gomora itastahimili zaidi katika hukumu kuliko mji huo.

Mateso Yanayokuja

16 “Tazama, ninawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Kwa hiyo mwe werevu kama nyoka na wapole kama hua.

17 “Jihadharini na wanadamu, kwa maana watawapeleka katika mabaraza yao na kuwapiga kwenye masinagogi yao, 18 nanyi mtaburutwa mbele ya watawala na wafalme kwa ajili yangu, ili kuwa ushuhuda kwao na mbele ya watu Mataifa. 19 Lakini watakapowapeleka humo, msisumbuke kufikirifikiri mtakalosema, kwa maana mtapewa la kusema wakati huo. 20 Kwa sababu si ninyi mtakaokuwa mkinena, bali ni Roho wa Baba yenu atakayekuwa akinena kupitia kwenu.

21 “Ndugu atamsaliti ndugu yake ili auawe na baba atamsaliti mtoto wake, watoto wataasi dhidi ya wazazi wao na kuwafanya wauawe. 22 Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. Lakini yeye atakayevumilia hadi mwisho ataokoka. 23 Wakiwatesa katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Amin, amin nawaambia, hamtamaliza miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Adamu kuja.

24 “Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake wala mtumishi hamzidi bwana wake. 25 Yatosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake na mtumishi kuwa kama bwana wake. Ikiwa mkuu wa nyumba ameitwa Beelzebuli
10.25 Beelzebuli kwa Kiyunani ni Beelzebubu, yaani mkuu wa pepo wachafu
, je, si zaidi sana wale wa nyumbani mwake mwenyewe!

Anayestahili Kuogopwa

26 “Kwa hiyo msiwaogope hao, kwa maana hakuna kilichofichika ambacho hakitafunuliwa, wala hakuna siri ambayo haitajulikana. 27 Ninalowaambia gizani, ninyi lisemeni mchana peupe na lile mnalosikia likinong'onwa, masikioni mwenu, lihubirini kwenye paa la nyumba. 28 Msiwaogope wale wauao mwili lakini hawawezi kuua roho. Afadhali, mwogopeni yeye awezaye kuiangamiza roho na mwili katika jehanamu
10.28 Jehanamu kwa Kiyunani ni Gehena, maana yake ni Kuzimu, yaani motoni
29 Je, shomoro wawili hawauzwi kwa senti mbili tu? Lakini hakuna hata mmoja wao atakayeanguka pasipo Baba yenu kujua. 30 Hata nywele za vichwa vyenu zote zimehesabiwa. 31 Hivyo msiogope, kwa maana ninyi ni wa thamani kubwa zaidi kuliko shomoro wengi.

32 “Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, mimi nami nitamkiri yeye mbele za Baba yangu aliye mbinguni. 33 Lakini ye yote atakayenikana mimi mbele ya watu, mimi nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.”

Sikuleta Amani, Bali Upanga

34 “Msidhani kwamba nimekuja kuleta amani duniani. Sikuja kuleta amani bali upanga. 35 Kwa maana nimekuja kumfitini “ ‘mtu na babaye,
binti na mamaye,
mkwe na mama mkwe wake;
36 nao adui za mtu watakuwa
ni wale watu wa nyumbani kwake.’37 “Ye yote ampendaye baba yake au mama yake kuliko anavyonipenda mimi, hastahili kuwa wangu. Ye yote ampendaye mwanawe au binti yake kuliko anavyonipenda Mimi, hastahili kuwa wangu. 38 Tena ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata, hastahili kuwa wangu. 39 Ayang'ang'aniaye maisha yake atayapoteza, lakini yeye atakayeyatoa maisha yake kwa ajili yangu atayapata.

Watakaopokea Thawabu

40 “Mtu ye yote atakayewapokea ninyi atakuwa amenipokea mimi na ye yote atakayenipokea mimi atakuwa amempokea yeye aliyenituma. 41 Mtu ye yote anayempokea nabii kwa kuwa ni nabii, atapokea thawabu ya nabii na mtu anayempokea mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapokea thawabu ya mwenye haki. 42 Kama ye yote akimpa hata kikombe cha maji mmoja wa hawa wadogo kwa kuwa ni mwanafunzi wangu, amin, ninawaambia, hataikosa thawabu yake.”

Copyright information for Neno