Matthew 12

Bwana Wa Sabato

Wakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya ngano siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, wakaanza kuvunja masuke ya ngano na kuyala. Lakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali siku ya Sabato.”

Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? Aliingia katika nyumba ya Mungu akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. Au hamjasoma katika Torati kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? Nawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. Kama mngelikuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Ninataka rehema, wala si dhabihu,’ msingeliwalaumu watu wasio na hatia, kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Yesu Anamponya Mtu Aliyepooza Mkono

Yesu akaondoka mahali hapo, akaingia katika sinagogi lao, 10 huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamwuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”

11 Yesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? 12 Mtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”

13 Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. 14 Lakini Mafarisayo wakatoka nje wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumwua.

Mtumishi Aliyechaguliwa Na Mungu

15 Lakini Yesu alipoyatambua mawazo yao, akaondoka mahali hapo. Watu wengi wakamfuata, naye akawaponya wote, 16 akiwakataza wasiseme yeye ni nani. 17 Hii ilikuwa ili litimie lile neno lililonenwa kwa kinywa cha nabii Isaya kusema: 18 “Tazama mtumishi wangu niliyemchagua,
mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Nitaweka Roho yangu juu yake,
naye atatangaza haki kwa mataifa.
19 Hatagombana wala hatapiga kelele,
wala hakuna atakayesikia sauti yake njiani.
20 Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
utambi unaofuka moshi hatauzima,
mpaka atakapoifanya haki ishinde.
21 Katika Jina lake mataifa
wataweka tumaini lao.”


Yesu Na Beelzebuli

22 Kisha wakamletea mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye ni kipofu na bubu, Yesu akamponya, hata akaweza kusema na kuona. 23 Watu wote wakashangaa na kusema, “Je, yawezekana huyu ndiye Mwana wa Daudi?”

24 Lakini Mafarisayo waliposikia jambo hili wakasema, “Mtu huyu anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa Beelzebuli
12.24 Beelzebuli au Beelzebubu; pia 12:27
, mkuu wa pepo wachafu.”

25 Yesu alijua walichokuwa wakiwaza, akawaambia, “Kila ufalme ukigawanyika dhidi yake wenyewe huangamia. Hali kadhalika kila mji au watu wa nyumba moja iliyogawanyika dhidi yake yenyewe haiwezi kusimama. 26 Kama Shetani akimtoa Shetani, atakuwa amegawanyika yeye mwenyewe. Basi ufalme wake utawezaje kusimama? 27 Nami kama natoa pepo wachafu kwa nguvu za Beelzebuli, watu wenu je, wao hutoa pepo wachafu kwa uwezo wa nani? Hivyo basi, wao ndio watakaowahukumu. 28 Lakini kama mimi ninatoa pepo wachafu kwa Roho wa Mungu, basi Ufalme wa Mungu umekuja juu yenu.

29 “Au tena, mtu awezaje kuingia katika nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuteka nyara mali zake asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Akishamfunga, ndipo hakika anaweza kuteka nyara mali zake.

30 “Mtu asiyekuwa pamoja nami yu kinyume nami na mtu ambaye hakusanyi pamoja nami, hutawanya. 31 Kwa hiyo nawaambia, kila dhambi na kufuru watu watasamehewa, lakini mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. 32 Mtu ye yote atakayesema neno dhidi ya Mwana wa Adamu atasamehewa, lakini ye yote anenaye neno dhidi ya Roho Mtakatifu hatasamehewa, iwe katika ulimwengu huu au katika ulimwengu ujao.

Mti Na Matunda yake

33 “Ufanye mti kuwa mzuri nayo matunda yake yatakuwa mazuri, au ufanye mti kuwa mbaya na matunda yake yatakuwa mabaya, kwa maana mti hutambulikana kwa matunda yake. 34 Enyi uzao wa nyoka! Mnawezaje kunena mambo mema, wakati ninyi ni waovu? Kwa maana kinywa cha mtu huyanena yale yaliyoujaza moyo wake. 35 Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina ya mambo mema yaliyohifadhiwa ndani yake, naye mtu mwovu hutoa yaliyo maovu kutoka katika hazina ya mambo maovu yaliyohifadhiwa ndani yake. 36 Lakini nawaambia, katika siku ya hukumu watu watatoa hesabu kuhusu kila neno lisilo maana walilonena. 37 Kwa maana kwa maneno yako utahesabiwa haki na kwa maneno yako utahukumiwa.”

Ishara Ya Yona

38 Kisha baadhi ya Mafarisayo na walimu wa sheria wakamwambia, “Mwalimu, tunataka kuona ishara kutoka kwako.”

39 Lakini yeye akawajibu, “Kizazi kiovu na cha uzinzi kinaomba ishara! Lakini hakitapewa ishara yo yote isipokuwa ile ishara ya nabii Yona. 40 Kwa maana kama vile Yona alivyokuwa ndani ya tumbo la nyangumi
12.40 Nyangumi ni samaki mkubwa sana
kwa muda wa siku tatu mchana na usiku, vivyo hivyo Mwana wa Adamu atakuwa katika moyo wa nchi siku tatu, mchana na usiku.
41 Siku ya hukumu watu wa Ninawi watasimama pamoja na kizazi hiki na kukihukumu, kwa maana wao walitubu katika kuhubiri kwa Yona na tazama hapa yupo yeye aliye mkuu kuliko Yona. 42 Malkia wa Kusini atasimama wakati wa hukumu na kukihukumu kizazi hiki, kwa kuwa yeye alikuja kutoka miisho ya dunia ili kuisikiliza hekima ya Solomoni na hapa yupo aliye mkuu kuliko Solomoni.”

Mafundisho Kuhusu Pepo Mchafu

43 “Pepo mchafu amtokapo mtu, hutangatanga katika sehemu zisizo na maji akitafuta mahali pa kupumzika, lakini hapati. 44 Ndipo husema, ‘Nitarudi kwenye ile nyumba yangu nilikotoka,’ Naye arudipo huikuta ile nyumba ikiwa tupu, imefagiliwa na kupangwa vizuri. 45 Kisha huenda na kuwaleta pepo wachafu wengine saba, wabaya zaidi kuliko yeye, nao huingia na kuishi humo. Nayo hali ya mwisho ya mtu yule huwa mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki cha uovu.”

Mama Na Ndugu zake Yesu

46 Wakati alipokuwa angali anazungumza na makutano, mama yake na ndugu zake walisimama nje wakitaka kuongea naye. 47 Ndipo mtu mmoja akamwambia, “Tazama mama Yako na ndugu Zako wamesimama nje, wanataka kuongea na wewe.”

48 Lakini yeye akamjibu na kumwambia yule mtu, “Mama yangu ni nani, nao ndugu zangu ni nani?” 49 Akiwanyoshea mkono wanafunzi wake, akasema, “Hawa hapa ndio mama yangu na ndugu Zangu! 50 Kwa maana ye yote afanyaye mapenzi ya Baba yangu wa mbinguni, ndiye ndugu yangu, dada yangu na mama yangu.”

Copyright information for Neno