Matthew 17

Yesu Abadilika Sura Mlimani

1Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, na kuwaleta mpaka juu ya mlima mrefu mahali pasipo na watu. 2Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang'aa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho. 3Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.

4Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”

5Petro alipokuwa angali ananena, ghafula, wingu linalong'aa likawafunika na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni mwanangu mpendwa, ninayependezwa naye sana, msikilizeni yeye.”

6Wale wanafunzi, waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu. 7Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.” 8Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine ye yote isipokuwa Yesu.

9Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu ye yote maono haya mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuka kutoka kwa wafu.”

10Wale wanafunzi wakamwuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria wanasema kwamba lazima Eliya aje kwanza?”

11Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya lazima aje kwanza naye atatengeneza mambo yote. 12Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.” 13Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yohana Mbatizaji.

Yesu Amponya Kijana Mwenye Pepo

14Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15“Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16Nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumponya.”

17Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi hata lini, nami nitawavumilia hadi lini? Mleteni kijana hapa kwangu.” 18Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.

19Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakati ambapo hakuna watu, wakamwuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”

20Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani kama punje ndogo ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu.” 21“Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.”

22Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa mikononi mwa watu. 23Nao watamwua na siku ya tatu atafufuka.” Wanafunzi wakahuzunika sana.

Yesu Na Petro Watoa Kodi Ya Hekalu

24Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu
17.24 Kodi ya Hekalu ilikuwa didrachmas, yaani drakma mbili, ambazo ni sawa na nusu shekeli
wakamjia Petro na kumwuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

25Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamwuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

26Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua, fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

Copyright information for Neno