Matthew 19

Yesu Afundisha Kuhusu Talaka

1Yesu alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Uyahudi, ng'ambo ya Mto Yordani. 2Umati mkubwa wa watu ukamfuata, naye akawaponya huko.

3Baadhi ya Mafarisayo wakamjia ili kumjaribu wakamwuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yo yote?”

4Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mtu mume na mtu mke. 5Naye akasema, ‘Kwa sababu hii mtu atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja?’ 6Hivyo si wawili tena, bali ni mwili mmoja. Kwa hiyo kile alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”

7Wakamwuliza, “Kwa nini basi Mose aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”

8Yesu akawajibu, “Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9Mimi nawaambia, ye yote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”

10Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”

11Yesu akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu 12Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine wamefanywa matowashi na wanadamu, na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya Ufalme wa Mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”

Yesu Awabariki Watoto Wadogo

13Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Yesu ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.

14Yesu akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” 15Naye akaweka mikono yake juu yao, akaondoka huko.

Kijana Tajiri

16Mtu mmoja akamjia Yesu na kumwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”

17Yesu akamjibu, “Mbona unaniita mimi mwema? Hakuna aliye mwema ila Mmoja tu, ndiye Mungu: Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”

18Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?”

Yesu akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo,
19waheshimu baba yako na mama yako na umpende jirani yako kama nafsi yako.”

20Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”

21Yesu akamwambia, “Kama ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”

22Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

Hatari Za Utajiri

23Ndipo Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Amin, amin nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mbinguni. 24Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu.”

25Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”

26Lakini Yesu akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote yanawezekana.”

27Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata, tutapata nini basi?”

28Yesu akawaambia, “Amin, amin nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, wakati Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake cha utukufu cha enzi, ninyi mliomfuata pia mtaketi katika viti vya enzi kumi na viwili, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29Kila mmoja aliyeacha nyumba au ndugu zake wa kiume au wa kike au baba au mama au watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo na ataurithi uzima wa milele. 30Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, nao walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Copyright information for Neno