Matthew 23

Yesu Awashutumu Walimu Wa Sheria Na Mafarisayo

1Kisha Yesu akauambia ule umati wa watu pamoja na wanafunzi wake: 2“Walimu wa sheria na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Mose, 3hivyo inawapasa kuwatii na kufanya kila kitu wanachowaambia. Lakini msifuate yale wanayotenda, kwa sababu hawatendi yale wanayohubiri. 4Wao hufunga mizigo mikubwa na kuiweka mabegani mwa watu, lakini wao wenyewe hawako radhi hata kuinua kidole ili kuisogeza.

5“Wao hutenda mambo yao yote ili waonekane na watu. Hufanya vikasha vya ngozi vyenye maandiko ya sheria na kurefusha matamvua ya mavazi yao, 6wanapenda kukaa viti vya sehemu za heshima karamuni na vile viti maalum sana katika masinagogi, 7hupenda kusalimiwa masokoni na kutaka watu wawaite ‘Rabi
23.7 Rabi maana yake Bwana, Mwalimu
.’

8“Lakini ninyi msiitwe ‘Rabi’ kwa sababu mnaye Bwana mmoja na ninyi nyote ni ndugu. 9Nanyi msimwite mtu ye yote ‘Baba,’ hapa duniani kwa maana mnaye Baba mmoja, naye yuko mbinguni. 10Wala msiitwe ‘Mwalimu,’ kwa maana mnaye mwalimu mmoja tu, ndiye Kristo
23:10 Yaani Masiya
.
11Yeye aliye mkuu kuliko ninyi nyote miongoni mwenu atakuwa mtumishi wenu. 12Kwa kuwa ye yote anayejikweza atashushwa na ye yote anayejinyenyekeza atakwezwa.

13“Lakini ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Kwa maana mnawafungia watu milango ya Ufalme wa Mbinguni. Ninyi wenyewe hamuingii humo, nao wale wanaotaka kuingia mnawazuia. [ 14Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, enyi wanafiki! Mnakula katika nyumba za wajane, nanyi kwa kujifanya kuwa wema, mnasali sala ndefu. Kwa hiyo adhabu yenu itakuwa kubwa zaidi.]

15“Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, wanafiki! Ninyi mnasafiri baharini na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja ageuke na kuwafuata ninyi, lakini baada ya kumpata, mnamfanya mwana wa jehanamu mara mbili kuliko ninyi!

16“Ole wenu, viongozi vipofu! Ninyi mwasema, ‘Mtu akiapa kwa Hekalu, kiapo hicho si kitu, lakini mtu akiapa kwa dhahabu ya Hekalu, amefungwa kwa kiapo chake.’ 17Ninyi vipofu wapumbavu! Ni kipi kilicho kikuu zaidi, ile dhahabu au lile Hekalu ambalo ndilo linaloifanya hiyo dhahabu kuwa takatifu? 18Pia mnasema, ‘Mtu akiapa kwa madhabahu, si kitu, lakini mtu akiapa kwa sadaka iliyo juu ya madhabahu, amefungwa kwa kiapo chake’ 19Ninyi vipofu! Ni kipi kikuu zaidi, ile sadaka, au ile madhabahu ambayo ndiyo inayoifanya hiyo sadaka kuwa takatifu? 20Kwa hiyo, mtu aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo madhabahu na vitu vyote vilivyo juu yake. 21Naye mtu aapaye kwa Hekalu, huapa kwa hilo Hekalu na kwa huyo akaaye ndani yake. 22Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu na kwa yeye aketiye juu ya kiti hicho.

23“Ole wenu walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnatoa zaka ya mnanaa, bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu zaidi ya sheria, yaani, haki, huruma na uaminifu. Haya imewapasa kuyafanya bila kusahau hayo mengine. 24Ninyi viongozi vipofu, mnachuja kiroboto lakini mnameza ngamia!

25“Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Kwa maana mnasafisha nje ya kikombe na kisahani, lakini ndani mmejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi. 26Enyi Mafarisayo vipofu! Safisheni kwanza ndani ya kikombe na kisahani, ndipo nje patakuwa safi.

27“Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnafanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, ambayo yanapendeza kwa nje lakini ndani yamejaa mifupa ya wafu na kila aina ya uchafu. 28Vivyo hivyo, kwa nje ninyi mnaonekana kwa watu kuwa wenye haki, lakini kwa ndani mmejaa unafiki na uovu.

29“Ole wenu, walimu wa sheria na Mafarisayo, ninyi wanafiki! Mnajenga makaburi ya manabii na kuyapamba makaburi ya wenye haki. 30Nanyi mwasema, ‘Kama tungaliishi wakati wa baba zetu, tusingalikuwa tumeshiriki katika kumwaga damu ya manabii!’ 31Hivyo mnajishuhudia wenyewe kwamba ninyi ni wana wa wale waliowaua manabii. 32Haya basi, kijazeni kipimo cha dhambi ya baba zenu!

33“Ninyi nyoka, ninyi uzao wa nyoka wenye sumu! Mtaiepukaje hukumu ya jehanamu? 34Kwa sababu hii tazama nawapelekea manabii na wenye hekima na walimu. Baadhi yao mtawaua na kuwasulibisha, wengine mtawapiga mijeledi katika masinagogi yenu na wengine mtawafuatia kutoka mji mmoja hadi mji mwingine. 35Hivyo ile damu ya wenye haki wote iliyomwagwa hapa duniani, tangu damu ya Abeli, ambaye alikuwa hana hatia, hadi damu ya Zekaria mwana wa Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu, itawajia juu yenu. 36Amin, nawaambia, haya yote yatakuja juu ya kizazi hiki.

Yesu Aililia Yerusalemu

37“Ee Yerusalemu, mnaowaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwenu! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! 38Tazama nyumba yako imeachwa tupu na ukiwa. 39Kwa maana nawaambia, hamtaniona tena mpaka siku ile mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana.’ ”

Copyright information for Neno