Matthew 28

Yesu Afufuka

Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.

Ghafula pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni akaenda penye kaburi akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.

Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njoni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtakakomwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”

Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini, wakiwa wamejawa na hofu lakini wenye furaha nyingi, wakaenda mbio ili kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. Ghafula Yesu akakutana nao, akasema, “salamu!” Wale wanawake wakamkaribia wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10 Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”

Taarifa Ya Walinzi

11 Wakati wale wanawake wakiwa njiani wakienda, baadhi ya wale askari waliokuwa wakilinda kaburi walienda mjini na kuwaeleza viongozi wa makuhani kila kitu kilichokuwa kimetukia. 12 Baada ya viongozi wa makuhani kukutana na wazee na kutunga hila, waliwapa wale askari kiasi kikubwa cha fedha 13 wakiwaambia, “Inawapasa mseme, ‘Wanafunzi wake walikuja wakati wa usiku na kumwiba sisi tulipokuwa tumelala.’ 14 Kama habari hizi zikimfikia mtawala, sisi tutamwondolea mashaka nanyi hamtapata tatizo lo lote.” 15 Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha nao wakafanya kama walivyoelekezwa. Habari hii imeenea miongoni mwa Wayahudi mpaka leo.

Yesu Awatuma Wanafunzi Wake

16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. 17 Walipomwona, wakamwabudu, lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.” Amen.

Copyright information for Neno