Matthew 6

Kuwapa Wahitaji

1“Angalieni msitende wema wenu mbele ya watu ili wawaone. Kwa maana mkifanya hivyo, hamna thawabu kutoka kwa Baba yenu aliye mbinguni.

2“Hivyo mnapowapa wahitaji, msipige panda mbele yenu kama wafanyavyo wanafiki katika masinagogi na mitaani, ili wasifiwe na watu. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupokea thawabu yao. 3Lakini ninyi mtoapo sadaka, fanyeni kwa siri, hata mkono wako wa kushoto usijue mkono wako wa kuume unachofanya, 4ili sadaka yako iwe ni siri. Ndipo Baba yako wa mbinguni, yeye aonaye sirini atakupa thawabu kwa wazi.

Kuhusu Maombi

5“Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu. Amin, amin nawaambieni, wao wamekwisha kupata thawabu yao. 6Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako. 7Nanyi mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. 8Msiwe kama wao, kwa sababu Baba yenu anajua kile mnachohitaji kabla hamjamwomba.

9“Hivi basi, ndivyo iwapasavyo kuomba: “ ‘Baba yetu uliye mbinguni,
Jina lako litukuzwe.
10Ufalme wako uje.
Mapenzi yako yafanyike
hapa duniani kama huko mbinguni.
11Utupatie leo riziki zetu
za kila siku.
12Utusamehe deni zetu,
kama sisi nasi tulivyokwisha
kuwasamehe wadeni wetu.
13Usitutie majaribuni,
bali utuokoe kutoka kwa yule mwovu
[kwa kuwa Ufalme ni wako na nguvu
na utukufu, hata milele. Amen].’


14Kwa kuwa kama mkiwasamehe watu wengine wanapowakosea, Baba yenu wa mbinguni atawasamehe na ninyi pia. 15Lakini msipowasamehe watu wengine makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Kuhusu Kufunga

16“Mnapofunga, msiwe wenye huzuni kama wafanyavyo wanafiki. Maana wao hukunja nyuso zao ili kuwaonyesha wengine kwamba wamefunga. Amin, amin nawaambia wao wamekwisha kupata thawabu yao kamilifu. 17Lakini mnapofunga, jipakeni mafuta kichwani na kunawa nyuso zenu 18ili kufunga kwenu kusionekane na watu wengine ila Baba yenu aketiye mahali pa siri, naye Baba yenu aonaye sirini atawapa thawabu yenu kwa wazi.

Akiba Ya Mbinguni

19“Msijiwekee hazina duniani, mahali ambapo nondo na kutu huharibu, nao wevi huvunja na kuiba. 20Lakini jiwekeeni hazina mbinguni, mahali ambapo nondo na kutu haviharibu, wala wevi hawavunji na kuiba. 21Kwa sababu mahali hazina yako ilipo, hapo ndipo pia moyo wako utakapokuwa.

Jicho Ni Taa Ya Mwili

22“Jicho ni taa ya mwili. Kama jicho lako ni nyofu, mwili wako wote utakuwa na nuru. 23Lakini kama jicho lako ni ovu, mwili wako wote utajawa na giza. Kwa hiyo basi, kama nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza, hilo ni giza kuu namna gani!

Mungu Na Mali

24“Hakuna mtu ye yote awezaye kuwatumikia mabwana wawili, kwa kuwa ama atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau huyu mwingine. Ninyi hamwezi kumtumikia Mungu na Mali
6.24 Mali (au Utajiri) hapa inatoka neno Mamoni kwa Kiaramu au Mamona kwa Kiyunani
.

Msiwe Na Wasiwasi

25“Kwa hiyo nawaambia, msiwe na wasiwasi kuhusu maisha yenu: mtakula nini au mtakunywa nini, au kuhusu miili yenu, mtavaa nini. Je, maisha si zaidi ya chakula na mwili zaidi ya mavazi? 26Waangalieni ndege wa angani, wao hawapandi wala hawavuni au kuweka ghalani, lakini Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Je, ninyi si wa thamani zaidi kuliko hao ndege? 27Ni nani miongoni mwenu ambaye kwa kujitaabisha kwake aweza kujiongezea hata saa moja zaidi katika maisha yake au kuongeza dhiraa moja
6.27 Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45
kwenye kimo chake?

28“Nanyi kwa nini kujitaabisha kwa ajili ya mavazi? Fikirini maua ya shambani yameavyo. Hayafanyi kazi wala hayafumi. 29Lakini nawaambia, hata Mfalme Solomoni katika fahari yake yote hakuvikwa kama mojawapo ya hayo maua. 30Lakini ikiwa Mungu anayavika hivi majani ya shambani, ambayo leo yapo na kesho yanatupwa motoni, je, hatawavika ninyi vizuri zaidi, enyi wa imani haba? 31Kwa hiyo msiwe na wasiwasi, mkisema, ‘Tutakula nini?’ Au ‘Tutakunywa nini?’ Au ‘Tutavaa nini?’ 32Kwa maana watu wasiomjua Mungu ndio wanaoshindania hayo, lakini Baba yenu wa mbinguni anafahamu kwamba mnahitaji hayo yote. 33Lakini utafuteni kwanza Ufalme wa Mungu na haki yake na haya yote mtaongezewa. 34Kwa hiyo msiwe na wasiwasi kuhusu kesho, kwa sababu kesho itajitaabikia yenyewe. Yatosha kwa siku masumbufu yake.

Copyright information for Neno