Matthew 26

Shauri Baya La Kumwua Yesu

1Yesu alipomaliza kusema hayo yote, akawaambia wanafunzi wake, 2“Mnajua kwamba baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, naye Mwana wa Adamu atasalitiwa ili asulibiwe.”

3Basi viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakakusanyika katika jumba la utawala la Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa. 4Wakafanya shauri ili kumkamata Yesu kwa siri na kumwua. 5Lakini wakasema, “Isiwe wakati wa sikukuu, la sivyo kutakuwa na ghasia miongoni mwa watu.”

Yesu Anapakwa Mafuta Huko Bethania

6Wakati Yesu akiwa Bethania nyumbani mwa Simoni aliyekuwa na ukoma, 7mwanamke mmoja alimjia akiwa na chupa ya marumaru yenye manukato ya thamani kubwa, akayamimina kichwani mwa Yesu alipokuwa ameketi mezani kula chakula.

8Lakini wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, “Kwa nini ubadhirifu huu wote? 9Manukato haya yangeliuzwa kwa bei kubwa na fedha hizo wakapewa maskini.”

10Yesu akijua jambo hili, akawaambia, “Mbona mnamsumbua huyu mwanamke? Yeye amenitendea jambo zuri sana. 11Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote. 12Alipomiminia haya manukato kwenye mwili amefanya hivyo ili kuniandaa kwa ajili ya maziko yangu. 13Ninawaambia kweli, mahali po pote habari njema itakapohubiriwa ulimwenguni mwote, jambo hili alilofanya litatajwa pia, kwa ukumbusho wake.”

Yuda Akubali Kumsaliti Yesu

14Kisha mmojawapo wa wale kumi na wawili, aitwaye Yuda Iskariote, alikwenda kwa viongozi wa makuhani 15na kuuliza, “Mtanipa nini nikimtia Yesu mikononi mwenu?” Wakamlipa vipande thelathini vya fedha. 16Tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta wasaa mzuri wa kumsaliti Yesu.

Yesu Ala Pasaka Pamoja Na Wanafunzi

17Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu wanafunzi walimjia Yesu wakamwuliza, “Unataka tuandae wapi kwa ajili yako ili kuila Pasaka?”

18Akajibu, “Nendeni kwa mtu fulani huko mjini mkamwambie, ‘Mwalimu asema hivi: Saa yangu imekaribia, nitaiadhimisha Pasaka pamoja na wanafunzi wangu katika nyumba yako.’ ” 19Hivyo wanafunzi wakafanya kama vile Yesu, alivyokuwa amewaelekeza, nao wakaandaa Pasaka.

20Ilipofika jioni, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wale kumi na wawili. 21Nao walipokuwa wakila, Yesu akasema, “Amin, amin nawaambia, mmoja wenu atanisaliti.”

22Wakahuzunika sana, wakaanza kumwambia mmoja mmoja, “Je, ni mimi Bwana?”

23Yesu akawaambia, “Yule aliyechovya mkono wake katika bakuli pamoja nami, ndiye atakayenisaliti. 24Mwana wa Adamu yu aenda kama alivyoandikiwa. Lakini ole wake mtu yule amsalitiye Mwana wa Adamu. Ingelikuwa bora kwake kama asingelizaliwa!”

25Kisha Yuda, yule aliyemsaliti akasema, “Kweli, si mimi Rabi?”

Yesu akajibu, “Naam, wewe mwenyewe umesema.”

Kuanzishwa Kwa Meza Ya Bwana

26Walipokuwa wanakula, Yesu akachukua mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, “Twaeni, mle, huu ndio mwili wangu.”

27Kisha akachukua kikombe, akashukuru, akawapa akisema, “Nyweni nyote katika kikombe hiki. 28Hii ndiyo damu yangu ya Agano, ile imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29Lakini ninawaambia, tangu sasa sitakunywa tena kutoka katika uzao huu wa mzabibu, mpaka siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu.”

30Walipokwisha kuimba wimbo, wakatoka kwenda mlima wa Mizeituni.

Yesu Atabiri Petro Kumkana

31Kisha Yesu akawaambia, “Usiku wa leo ninyi nyote mtaniacha, kwa maana imeandikwa: “ ‘Nitampiga mchungaji,
nao kondoo wa hilo kundi watatawanyika.’


32Lakini baada ya mimi kufufuka, nitawatangulia kwenda Galilaya.”

33Petro akajibu “Hata kama wote watakuacha, kamwe mimi sitakuacha.”

34Yesu akajibu, “Amin, amin ninakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.”

35Lakini Petro akasema, “Hata kama itabidi kufa pamoja na wewe, kamwe sitakukana.” Nao wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.

Yesu Anaomba Gethsemane

36Kisha Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka kwenye bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda kule kuomba.” 37Akamchukua Petro pamoja na wale wana wawili wa Zebedayo, naye akaanza kuhuzunika na kufadhaika. 38Kisha Yesu akawaambia, “Moyo wangu umejawa na huzuni kiasi cha kufa. Kaeni hapa na mkeshe pamoja nami.”

39Akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi akaomba, akisema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki na kiniepuke, lakini si kama nitakavyo mimi bali kama utakavyo wewe.”

40Kisha akarudi kwa wanafunzi wake na kuwakuta wamelala. Akamwuliza Petro, “Je, ninyi wanaume, hamkuweza kukesha pamoja nami kwa saa moja? 41Kesheni na muombe, msije mkaanguka majaribuni. Hakika roho iko radhi lakini mwili ni dhaifu.”

42Akaenda tena mara ya pili na kuomba, “Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisikinywe, basi mapenzi yako yafanyike.”

43Aliporudi, akawakuta tena wamelala kwa sababu macho yao yalikuwa mazito. 44Hivyo akawaacha akaenda zake tena mara ya tatu na kuomba akisema maneno yale yale.

45Kisha akarudi kwa wanafunzi wake akawaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Tazameni, saa imefika ambapo Mwana wa Adamu hana budi kutiwa mikononi mwa wenye dhambi. 46Inukeni, twendeni zetu! Huyu hapa yule anisalitiye!”

Yesu Akamatwa

47Alipokuwa bado anasema, Yuda, mmojawapo wa wale Kumi na Wawili, akafika, akiwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara kwamba: “yeye nitakayembusu ndiye, mkamateni.” 49Mara akamjia Yesu na kumsalimu, “salamu, Rabi!” Akambusu.

50Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”

Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu.
51Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

52Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga. 53Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54Lakini je, maandiko yatatimiaje yale yasemayo kwamba ni lazima itokee hivi?”

55Wakati huo Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Mmetoka na panga na marungu kuja kunikamata kama vile mimi ni mnyang'anyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata? 56Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.

Yesu Mbele Ya Kuhani Mkuu

57Wale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika. 58Lakini Petro akamfuata kwa mbali mpaka uani kwa Kuhani Mkuu. Akaingia ndani akaketi pamoja na walinzi ili aone litakalotukia.

59Basi viongozi wa wazee, makuhani na baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumwua. 60Lakini hawakupata jambo lo lote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo
61na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

62Kisha Kuhani Mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi wa namna gani hawa watu wauletao dhidi yako?” 63Lakini Yesu alikuwa kimya.

Ndipo Kuhani Mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai, tuambie ikiwa wewe ndiwe Kristo
26:63 Yaani Masiya, pia 68
, Mwana wa Mungu.”

64Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote, tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65Ndipo Kuhani Mkuu akararua nguo zake na kusema, “Amekufuru! Kwa nini tunahitaji ushahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru. 66Uamuzi wenu ni nini?”

Wakajibu, “Anastahili kufa.”

67Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine walimpiga makofi 68na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

Petro Amkana Bwana Yesu

69Wakati huu Petro alikuwa amekaa nje uani. Mtumishi mmoja wa kike akamjia na kumwambia, “Wewe pia ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya.”

70Lakini Petro akakana mbele yao wote akisema, “Sijui hilo usemalo.”

71Alipotoka nje kufika kwenye lango, mtumishi mwingine wa kike alimwona, akawaambia watu waliokuwapo, “Huyu mtu alikuwa pamoja na Yesu, Mnazareti.”

72Akakana tena kwa kiapo akisema, “Mimi simjui huyo!”

73Baada ya muda mfupi wale waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro wakamwambia, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana ile namna yako ya kusema ni kama yao.”

74Ndipo Petro akaanza kujilaani na kuwaapia, “Mimi simjui mtu huyo!”

Papo hapo jogoo akawika.
75Ndipo Petro akakumbuka lile neno alilokuwa amesema Yesu, “Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu.” Akaenda nje, akalia sana.

Copyright information for Neno