Matthew 27

Yesu Aletwa Mbele Ya Pilato

1Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri pamoja dhidi ya Yesu ili kumwua. 2Wakamfunga, wakampeleka na kumkabidhi kwa Pilato, ambaye alikuwa mtawala.

Yuda Ajinyonga

3Yuda, ambaye ndiye aliyekuwa amemsaliti Yesu, alipoona kuwa Yesu amehukumiwa, akajuta na akarudisha vile vipande thelathini vya fedha alivyopewa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 4Akasema, “Nimetenda dhambi, kwa maana nimeisaliti damu isiyo na hatia.”

5Basi Yuda akavitupa vile vipande vya fedha ndani ya Hekalu akaondoka akaenda kujinyonga.

6Wale makuhani wakuu wakazichukua zile fedha wakasema, “Si halali kuchanganya fedha hizi na sadaka kwa sababu hizi ni fedha zenye damu.” 7Kwa hiyo baada ya kushauriana, waliamua kuzitumia kununulia shamba la mfinyanzi, liwe mahali pa kuzikia wageni. 8Hii ndiyo sababu lile shamba likaitwa Shamba la Damu hadi leo. 9Ndipo likatimia lile lililonenwa na nabii Yeremia kwamba, “Walichukua vile vipande thelathini vya fedha, thamani aliyopangiwa na watu wa Israeli, 10wakanunulia shamba la mfinyanzi, kama vile Bwana alivyoniagiza.”

Yesu Mbele Ya Pilato

11Wakati Yesu akiwa amesimama mbele ya mtawala, mtawala akamwuliza, “Wewe ndiye mfalme wa Wayahudi?”

Yesu akasema, “Wewe wasema hivyo.”

12Lakini viongozi wa makuhani na wazee walipomshtaki, hakujibu neno. 13Ndipo Pilato akamwuliza, “Je, husikii ni mambo mangapi wanayokushtaki nayo?” 14Lakini Yesu hakumjibu hata kwa shtaka moja, kiasi kwamba mtawala alishangaa sana.

15Basi ilikuwa ni desturi ya mtawala kumfungua mfungwa mmoja atakayechaguliwa na umati wa watu wakati wa sikukuu. 16Wakati huo alikuwapo mfungwa mmoja mwenye sifa mbaya, aliyeitwa Baraba. 17Hivyo umati wa watu walipokusanyika, Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie nani, Baraba au Yesu yeye aitwaye Kristo?” 18Kwa kuwa alitambua Yesu alikuwa amekabidhiwa kwake kwa ajili ya wivu.

19Pilato akiwa ameketi kwenye kiti cha hukumu, mkewe akampelekea ujumbe huu: “Usiwe na jambo lo lote juu ya mtu huyu asiye na hatia, kwa kuwa leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake.”

20Lakini viongozi wa makuhani na wazee wakaushawishi ule umati wa watu kwamba waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.

21Mtawala akawauliza tena, “Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka niwafungulie?”

Wakajibu, “Baraba.”

22Pilato akawaambia, “Basi nifanye nini na huyu Yesu aitwaye Kristo?”

Wakajibu wote, “Msulibishe!”

23Pilato akauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”

Lakini wao wakazidi kupiga kelele, “Msulibishe.”

24Pilato alipoona kwamba hawezi kufanya lo lote, lakini badala yake ghasia zilikuwa zinaanza, akachukua maji, akanawa mikono yake mbele ya ule umati wa watu, akasema, “Sina hatia juu ya damu ya mtu huyu, hili ni jukumu lenu!”

25Watu wote wakajibu, “Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!”

26Basi akawafungulia Baraba na baada ya kumchapa Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.

Askari Wamdhihaki Yesu

27Kisha askari wa mtawala wakampeleka Yesu kwenye Praitorio
27.27 Praitorio maana yake makao makuu ya mtawala, jumba la kifalme lililokuwa linakaliwa na Pontio Pilato huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu
na wakakusanya kikosi kizima cha askari kumzunguka.
28Wakamvua nguo zake na kumvika vazi la rangi nyekundu, kisha 29wakasokota taji ya miiba wakaiweka kichwani pake. Wakamwekea fimbo katika mkono wake wa kuume, wakapiga magoti mbele zake na kumdhihaki wakisema “salamu, mfalme wa Wayahudi!” 30Wakamtemea mate, wakachukua ile fimbo wakampiga kichwani tena na tena. 31Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile vazi, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakampeleka ili kumsulibisha.

Yesu Asulibishwa

32Walipokuwa wakienda, wakakutana na mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 33Wakafika mahali paitwapo Golgotha (ambayo maana yake ni, Mahali pa Fuvu la Kichwa), 34wakampa Yesu divai iliyochanganywa na nyongo ili anywe, lakini alipoionja, akakataa kuinywa. 35Walipokwisha kumsulibisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura, [ili litimie lile neno lililonenwa na nabii, “Waligawa nguo zangu miongoni mwao na vazi langu wakalipigia kura.”] 36Kisha wakaketi, wakamchunga. 37Juu ya kichwa chake, kwenye msalaba, wakaandika shtaka lake: HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. 38Wanyang'anyi wawili walisulibiwa pamoja naye, mmoja kuume kwake na mwingine kushoto kwake. 39Watu waliokuwa wakipita njiani wakamvurumishia matukano huku wakitikisa vichwa vyao 40na kusema, “Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe mwenyewe basi! Kama wewe ni Mwana wa Mungu, shuka kutoka msalabani.”

41Vivyo hivyo, viongozi wa, makuhani, walimu wa sheria na wazee wakamdhihaki wakisema, 42“Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! Yeye ni Mfalme wa Israeli! Ashuke sasa kutoka msalabani, tutamwamini. 43Anamwamini Mungu, basi Mungu na amwokoe sasa kama anamtaka, kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’ ” 44Hata wale wanyang'anyi waliosulibiwa pamoja naye wakamtukana vivyo hivyo.

Kifo Cha Yesu

45Tangu saa sita hadi saa tisa giza lilifunika nchi yote. 46Ilipofika saa tisa Yesu akapaza sauti akalia,  “Eloi, Eloi lama Sabakthani?” Maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

47Baadhi ya wale watu waliokuwa wamesimama pale waliposikia haya, wakasema “Anamwita Eliya,”

48Ghafula mmoja wao akaenda mbio na kuleta sifongo akaichovya kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi akampa Yesu ili anywe. 49Wengine wakasema, “Mwacheni na tuone kama Eliya atakuja kumwokoa.”

50Yesu alipolia tena kwa sauti kuu, akaitoa roho yake.

51Wakati huo huo pazia la Hekalu likachanika vipande viwili, kuanzia juu hadi chini. Dunia ikatetemeka na miamba ikapasuka. 52Makaburi yakafunguka na miili ya watakatifu waliokuwa wamekufa ikafufuka. 53Wakatoka makaburini na baada ya Yesu kufufuka waliingia kwenye Mji Mtakatifu na kuwatokea watu wengi.

54Basi yule jemadari na wale waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu walipoona lile tetemeko na yale yote yaliyokuwa yametukia, wakaogopa wakasema, “Hakika huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu!”

55Walikuwako wanawake huko, wakiangalia kwa mbali. Hawa walikuwa wamemfuata Yesu tangu Galilaya ili kushughulika na mahitaji yake. 56Miongoni mwao walikuwapo Maria Magdalene, Maria mama yake Yakobo na Yosefu na mama yao wana wa Zebedayo.

Maziko Ya Yesu

57Ilipofika jioni, alifika mtu mmoja tajiri kutoka Arimathea aitwaye Yosefu, ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu. 58Akamwendea Pilato, kumwomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe. 59Yosefu akauchukua mwili wa Yesu, akauviringishia nguo ya kitani safi nyeupe 60na kuuzika kwenye kaburi lake mwenyewe jipya alilokuwa amelichonga kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mlangoni mwa kaburi, akaenda zake. 61Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwapo mahali pale, wakiwa wameketi mkabala na kaburi.

Walinzi Pale Kaburini

62Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalizi ya Sabato, viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakamwendea Pilato 63na kusema, “Bwana, tumekumbuka kwamba yule mdanganyifu kabla hajafa alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’ 64Kwa hiyo uamuru kaburi lilindwe kwa uthabiti mpaka baada ya siku tatu. La sivyo, wanafunzi wake wanaweza kuja kuuiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuka kutoka kwa wafu. Udanganyifu huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa kwanza.”

65Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari walinzi. Nendeni, liwekeeni ulinzi kadri mwezavyo.” 66Kwa hiyo wakaenda na walinzi ili kulilinda kaburi kwa uthabiti, wakatia muhuri kwenye lile jiwe na kuweka ulinzi.

Copyright information for Neno