Micah 6

Shauri La BWANA Dhidi Ya Israeli

1Sikiliza asemalo BWANA: “Simama, tetea shauri lako mbele ya milima;
vilima na visikie lile unalotaka kusema.
2Sikilizeni, Ee milima, mashtaka ya BWANA,
sikilizeni, enyi misingi ya milele ya dunia.
Kwa kuwa BWANA ana shauri dhidi ya watu wake;
anatoa mashtaka dhidi ya Israeli.
3“Watu wangu, nimewatendea nini?
Nimewalemea kwa jinsi gani? Mnijibu.
4Nimewatoa kutoka Misri na kuwakomboa
kutoka nchi ya utumwa.
Nilimtuma Mose awaongoze,
pia Aroni na Miriamu.
5Watu wangu, kumbukeni jinsi Balaki mfalme wa Moabu
alivyofanya shauri
na kile Balamu mwana wa Beori alichojibu.
Kumbukeni safari yenu kutoka Shitimu mpaka Gilgali,
ili mfahamu matendo ya haki ya BWANA.”
6Nimjie BWANA na kitu gani na kusujudu
mbele za Mungu aliyetukuka?
Je, nije mbele zake na sadaka za kuteketezwa,
nije na ndama za mwaka mmoja?
7Je, BWANA atafurahishwa na kondoo dume elfu,
au mito elfu kumi ya mafuta?
Je, nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa ajili ya kosa langu,
mtoto wangu mwenyewe
kwa ajili ya dhambi ya nafsi yangu?
8Amekuonyesha yaliyo mema, ee mwanadamu.
BWANA anataka nini kwako?
Ila kutenda kwa haki na kupenda rehema,
na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako.


Hatia Na Adhabu Ya Israeli

9Sikiliza! BWANA anauita mji:
kulicha jina lako ni hekima:
“Tii hiyo fimbo na yeye aliyeiamuru.
10Je, bado nisahau, Ee nyumba ya uovu,
hazina yako uliyopata kwa udanganyifu
na vipimo vilivyopunguka,
ambavyo vimelaaniwa?
11Je, naweza kuhukumu kuwa
mtu mwenye mizani ya udanganyifu hana hatia,
aliye na mfuko wa mawe ya kupimia ya uongo?
12Matajiri wake ni wajeuri;
watu wake ni waongo
na ndimi zao zinazungumza
kwa udanganyifu.
13Kwa hiyo, nimeanza kukuharibu,
kuwaangamiza kwa sababu ya dhambi zenu.
14Mtakula lakini hamtashiba;
matumbo yenu bado yatakuwa matupu.
Mtaweka akiba lakini hamtaokoa cho chote,
kwa sababu mtakachoweka akiba
nitatoa kwa upanga.
15Mtapanda lakini hamtavuna;
mtakamua zeituni lakini
hamtatumia mafuta yake.
Mtakamua zabibu
lakini hamtakunywa hiyo divai.
16Mmezishika sheria za Omri
na matendo yote ya nyumba ya Ahabu,
tena umefuata desturi zao.
Kwa hiyo nitakutoa kwa maangamizi
na watu wako kuwa dhihaka;
mtachukua dharau za mataifa.”
Copyright information for Neno