Numbers 16

Kora, Dathani Na Abiramu

1Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, pamoja na baadhi ya Wareubeni, yaani Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni mwana wa Palethi, wakachukua baadhi ya watu, 2wakainuka dhidi ya Mose. Pamoja nao walikuwapo wanaume wa Kiisraeli 250, watu waliojulikana, viongozi wa jumuiya waliokuwa wameteuliwa kuwa wakuu wa kusanyiko. 3Wakaja kama kikundi kuwapinga Mose na Aroni, wakawaambia, “Ninyi mmejitukuza sana! Kusanyiko hili lote ni takatifu, kila mmoja wao, naye BWANA yu pamoja nao. Kwa nini basi mmejitukuza wenyewe juu ya kusanyiko la BWANA?”

4Mose aliposikia jambo hili, akaanguka kifudifudi. 5Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake wote: “Asubuhi BWANA ataonyesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, tena atamtaka mtu huyo aje kwake. Mtu yule ambaye atamchagua atamfanya kuja karibu naye. 6Wewe Kora na wafuasi wako wote mtafanya hivi: Chukueni vyetezo, 7kesho wekeni moto na uvumba kwenye hivyo vyetezo mbele za BWANA. Mtu ambaye BWANA atamchagua atakuwa ndiye mtakatifu. Ninyi Walawi mmejitukuza sana!”

8Pia Mose akamwambia Kora, “Enyi Walawi! Sasa nisikilizeni. 9Haiwatoshi ninyi kwamba Mungu wa Israeli amewateua ninyi kutoka katika kusanyiko lote la Kiisraeli, na kuwaleta karibu naye mpate kufanya kazi kwenye Maskani ya BWANA, na kusimama mbele ya kusanyiko ili kuwahudumia? 10Amekuleta wewe na ndugu zako Walawi mwe karibu naye, lakini sasa unajaribu kupata na ukuhani pia. 11Wewe na wafuasi wako wote mmekusanyika pamoja kinyume cha BWANA. Aroni ni nani kwamba ninyi mnung'unike dhidi yake?”

12Kisha Mose akawaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu. Lakini wao wakasema, “Sisi hatuji! 13Haitoshi tu kwamba wewe umetuleta kutoka nchi itiririkayo maziwa na asali ili kutuua sisi jangwani? Nawe sasa pia unataka kuwa mkuu juu yetu? 14Zaidi ya hayo, hujatuingiza katika nchi inayotiririka maziwa na asali, wala hujatupa urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Je, utayang'oa macho ya watu hawa? Hapana, sisi hatuji!”

15Ndipo Mose akakasirika sana na kumwambia BWANA, “Usiikubali sadaka yao. Mimi sikuchukua cho chote, hata punda kutoka kwao, wala sijamkosea hata mmoja wao.”

16Mose akamwambia Kora, “Wewe na wafuasi wako wote kesho mtatokea mbele za BWANA, yaani wewe na hao wenzako, pamoja na Aroni. 17Kila mtu atachukua chetezo chake na kuweka uvumba ndani yake, vyetezo 250 kwa jumla na kuleta mbele za BWANA. Pia wewe na Aroni mtaleta vyetezo vyenu.” 18Kwa hiyo kila mtu akachukua chetezo chake, akaweka moto na uvumba ndani yake, na kusimama pamoja na Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania. 19Kora alipokuwa amekusanya wafuasi wake wote kuwapinga Mose na Aroni kwenye mlango wa Hema la Kukutania, utukufu wa BWANA ukatokea kwa kusanyiko lote. 20BWANA akamwambia Mose na Aroni, 21“Jitengeni kutoka kwenye kusanyiko hili ili nipate kuwaangamiza mara moja.”

22Lakini Mose na Aroni wakaanguka kufudifudi na kulia kwa sauti, wakasema, “Ee Mungu, Mungu wa roho za wanadamu wote, utakuwa na hasira na kusanyiko lote wakati ni mtu mmoja tu ametenda dhambi?”

23Ndipo BWANA akamwambia Mose, 24“Liambie kusanyiko, ‘Ondokeni hapo karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu.’ ”

25Mose akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu, nao wazee wa Israeli wakafuatana naye. 26Mose akalionya kusanyiko, “Sogeeni nyuma mbali na mahema ya hawa watu waovu! Msiguse kitu cho chote kilicho mali yao, la sivyo mtafagiliwa mbali kwa sababu ya dhambi zao zote.” 27Hivyo wakaondoka karibu na mahema ya Kora, Dathani na Abiramu. Dathani na Abiramu walikuwa wametoka nje, nao walikuwa wamesimama pamoja na wake zao, watoto wao na wale wanyonyao kwenye mlango wa mahema yao.

28Ndipo Mose akasema, “Hivi ndivyo mtakavyojua kuwa BWANA amenituma kufanya mambo haya, na kwamba halikuwa wazo langu. 29Ikiwa watu hawa watakufa kifo cha kawaida na kupatwa na yale ya kawaida yanayowapata wanadamu, basi BWANA hakunituma mimi. 30Lakini ikiwa BWANA ataleta jambo jipya kabisa, ardhi ikifunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na kila kitu kilicho mali yao, nao washuke chini kaburini
16.30 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol
wakiwa hai, ndipo mtafahamu kuwa watu hawa wamemdharau BWANA.”

31Mara Mose alipomaliza kusema haya yote, ardhi iliyokuwa chini yao ikapasuka, 32nchi ikafunua kinywa chake na kuwameza wao, pamoja na jamaa zao, na watu wote wa Kora na mali zao zote. 33Wakashuka chini kaburini wakiwa hai, pamoja na kila kitu walichokuwa nacho; nchi ikajifunika juu yao, nao wakaangamia wakatoweka kutoka katika kusanyiko. 34Kutoka kilio chao, Waisraeli wote waliowazunguka walikimbia, wakipaza sauti, “Nchi inatumeza na sisi pia!”

35Moto ukaja kutoka kwa BWANA, ukawateketeza wale watu 250 waliokuwa wakifukiza uvumba.

36BWANA akamwambia Mose, 37“Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni, atoe vyetezo kwenye mabaki ya moto na kutawanya makaa mbali kiasi, kwa maana vyetezo ni vitakatifu, 38vyetezo vya watu waliofanya dhambi iliyowagharimu maisha yao. Fua vyetezo hivyo kuwa bamba ili kufunika madhabahu, kwa maana vimeletwa mbele za BWANA na vimekuwa vitakatifu. Navyo viwe ishara kwa Waisraeli.”

39Hivyo kuhani Eleazari akavikusanya vile vyetezo vya shaba vilivyoletwa na wale waliokuwa wameteketezwa kwa moto, naye akavifua kufunika madhabahu, 40kama vile BWANA alivyomwelekeza kupitia Mose. Hili lilikuwa kuwakumbusha Waisraeli kwamba hakuna mtu hata mmoja, isipokuwa mzao wa Aroni, awezaye kuja kufukiza uvumba mbele za BWANA, la sivyo, angekuwa kama Kora na wafuasi wake.

41Siku iliyofuata jumuiya yote ya Kiisraeli wakanung'unika dhidi ya Mose na Aroni, wakisema, “Mmewaua watu wa BWANA.”

42Lakini wakati kusanyiko lilipokusanyika kupingana na Mose na Aroni, nalo likageuka kuelekea Hema la Kukutania, ghafula wingu likafunika Hema, nao utukufu wa BWANA ukatokea. 43Ndipo Mose na Aroni wakaenda mbele ya Hema la Kukutania, 44naye BWANA akamwambia Mose, 45“Jitenge mbali na kusanyiko hili ili niweze kuwaangamiza mara moja.” Wakaanguka chini kifudifudi.

46Kisha Mose akamwambia Aroni, “Chukua chetezo chako na uweke uvumba ndani yake, pamoja na moto kutoka madhabahuni, nawe uende haraka kwenye kusanyiko ili kufanya upatanisho kwa ajili yao. Ghadhabu imekuja kutoka kwa BWANA, na tauni imeanza.” 47Hivyo Aroni akafanya kama Mose alivyosema, akakimbilia katikati ya kusanyiko. Tauni ilikuwa tayari imeanza miongoni mwa watu, lakini Aroni akafukiza uvumba na kufanya upatanisho kwa ajili yao. 48Aroni akasimama kati ya waliokuwa hai na waliokufa, nayo tauni ikakoma. 49Lakini walikufa watu 14,700 kutokana na tauni hiyo, licha ya wale waliokuwa wamekufa kwa sababu ya Kora. 50Ndipo Aroni akamrudia Mose kwenye mlango wa Hema la Kukutania, kwa maana tauni ilikuwa imekoma.

Copyright information for Neno