Numbers 17

Kuchipuka Kwa Fimbo Ya Aroni

1BWANA akamwambia Mose, 2“Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa kabila za baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake. 3Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Aroni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao. 4Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe. 5Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manung'uniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”

6Hivyo Mose akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Aroni ikiwa miongoni mwa hizo. 7Mose akaziweka hizo fimbo mbele za BWANA ndani ya Hema la Ushuhuda.

8Siku iliyofuata Mose aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Aroni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi. 9Ndipo Mose akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za BWANA. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.

10BWANA akamwambia Mose, “Rudisha fimbo ya Aroni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manung'uniko yao dhidi yangu, ili kwamba wasife.” 11Mose akafanya sawasawa kama BWANA alivyomwamuru.

12Waisraeli wakamwambia Mose, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea! 13Ye yote akaribiaye Maskani ya BWANA atakufa. Je, sisi sote tutakufa?”

Copyright information for Neno