Numbers 2

Mpangilio Wa Kambi Za Makabila

BWANA aliwaambia Mose na Aroni: “Waisraeli watapiga kambi zao kuzunguka Hema la Kukutania kwa umbali fulani kutoka kwenye hema, kila mwanaume chini ya alama yake pamoja na bendera ya jamaa yake.”Kwa upande wa mashariki kuelekea maawio ya jua, kambi ya makundi ya Yuda watapiga kambi chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Yuda ni Nashoni mwana wa Aminadabu. Kundi lake lina watu 74,600.

Kabila la Isakari watapiga kambi karibu na Yuda. Kiongozi wa watu wa Isakari ni Nethaneli mwana wa Suari. Kundi lake lina watu 54,400.

Kabila la Zabuloni litafuata. Kiongozi wa watu wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. Kundi lake lina watu 57,400.

Wanaume wote walio katika kambi ya Yuda, kufuatana na makundi yao, ni 186,400. Wao watatangulia kwanza kuondoka.10 Kwa upande wa kusini kutakuwa kambi ya makundi ya Reubeni chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Reubeni ni Elisuri mwana wa Shedeuri. 11 Kundi lake lina watu 46,500.

12 Kabila la Simeoni watapiga kambi karibu na Reubeni. Kiongozi wa watu wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Surishadai. 13 Kundi lake lina watu 59,300.

14 Kabila la Gadi litafuata. Kiongozi wa watu wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. 15 Kundi lake lina watu 45,650.

16 Wanaume wote walio katika kambi ya Reubeni, kufuatana na makundi yao, ni 151,450. Nao watakuwa nafasi ya pili kuondoka.17 Kisha Hema la Kukutania na kambi ya Walawi vitakuwa katikati ya kambi zote. Wao watasafiri kwa utaratibu ule ule kama walivyopiga kambi, kila mmoja mahali pake mwenyewe chini ya alama yake.18 Upande wa magharibi kutakuwepo na kambi ya makundi ya Efraimu chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Efraimu ni Elishama mwana wa Amihudi. 19 Kundi lake lina watu 40,500.

20 Kabila la Manase litafuata baada ya Efraimu. Kiongozi wa watu wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. 21 Kundi lake lina watu 32,200.

22 Kabila la Benyamini litafuata baada ya Manase. Kiongozi wa watu wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. 23 Kundi lake lina watu 35,400.

24 Wanaume wote walio katika kambi ya Efraimu kufuatana na makundi yao ni 108,100. Nao watakuwa nafasi ya tatu kuondoka.25 Upande wa kaskazini kutakuwa na makundi ya kambi ya Dani, chini ya alama yao. Kiongozi wa watu wa Dani ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. 26 Kundi lake lina watu 62,700.

27 Kabila la Asheri watapiga kambi karibu na Dani. Kiongozi wa watu wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani. 28 Kundi lake lina watu 41,500.

29 Kabila la Naftali litafuata. Kiongozi wa watu wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. 30 Kundi lake lina watu 53,400.

31 Wanaume wote walio katika kambi ya Dani ni 157,600. Wao watakuwa wa mwisho kuondoka chini ya alama yao.32 Hawa ndio Waisraeli, wakiwa wamehesabiwa kufuatana na jamaa zao. Wote wale walio kambini kwa makundi yao ni watu 603,550. 33 Hata hivyo, Walawi hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine, kama BWANA alivyomwagiza Mose.34 Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kila kitu BWANA alichomwamuru Mose. Hivyo ndivyo walivyopiga kambi chini ya alama zao, pia hivyo ndivyo walivyoondoka, kila mmoja akiwa na ukoo wake na jamaa yake.

Copyright information for Neno