Numbers 27

Binti Wa Selofehadi

1Binti za Selofehadi mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, walikuwa wa koo za Manase mwana wa Yosefu. Majina ya hao binti yalikuwa Mahla, Noa, Hogla, Milka na Tirsa. Walikaribia 2ingilio la Hema la Kukutania na kusimama mbele ya Mose, kuhani Eleazari, viongozi na kusanyiko lote, wakasema, 3“Baba yetu alikufa jangwani. Hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora, ambao walifungamana pamoja dhidi ya BWANA, lakini alikufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe na hakuacha wana. 4Kwa nini jina la baba yetu lifutike kutoka katika ukoo wake kwa sababu hakuwa na mwana? Tupatie milki miongoni mwa ndugu za baba yetu.”

5Kwa hiyo Mose akalileta shauri lao mbele za BWANA, 6naye BWANA akamwambia, 7“Wanachosema binti za Selofehadi ni sawa, ni lazima kwa hakika uwape milki kama urithi miongoni mwa ndugu za baba yao, na kubadili urithi wa baba yao uwe wao.

8“Waambie Waisraeli, ‘Ikiwa mtu atakufa naye hakuacha mwana, utampa binti yake urithi wake. 9Ikiwa hana binti, wape ndugu zake wa kiume urithi wake. 10Ikiwa hana ndugu wa kiume toa urithi wake kwa ndugu za baba yake. 11Ikiwa baba yake hakuwa na ndugu wa kiume, toa urithi wake kwa ndugu wa karibu katika ukoo wake, ili aumiliki. Hili litakuwa dai la sheria kwa Waisraeli, kama BWANA alivyomwamuru Mose.’ ”

Yoshua Kuchukua Nafasi Ya Mose

12Kisha BWANA akamwambia Mose, “Panda juu ya mlima huu katika kilele cha Abarimu uione nchi ambayo nimewapa Waisraeli. 13Baada ya kuiona, wewe pia utakusanywa pamoja na watu wako kama ndugu yako Aroni alivyokusanywa, 14kwa kuwa jumuiya ilipoasi amri yangu kwenye maji katika Jangwa la Sini, wakati jumuiya ilipogombana nami, nyote wawili mliacha kuitii amri yangu ya kuniheshimu kama mtakatifu mbele ya macho yao.” (Haya yalikuwa maji ya Meriba huko Kadeshi, katika Jangwa la Sini.)

15Mose akamwambia BWANA, 16“BWANA, Mungu wa roho zote za wanadamu, na amteue mtu juu ya jumuiya hii 17ili atoke na kuingia mbele yao, atakayewaongoza katika kutoka kwao na kuingia kwao, ili watu wa BWANA wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.”

18Kwa hiyo BWANA akamwambia Mose, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho yuko ndani yake, uweke mkono juu yake. 19Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao. 20Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli ipate kumtii. 21Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za BWANA kwa ile Urimu
27:21 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha Kuhani Mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha
. Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.”

22Mose akafanya kama BWANA alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote. 23Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile BWANA alivyoelekeza kupitia kwa Mose.

Copyright information for Neno