Obadia

Obadia

Utangulizi

Jina Obadia maana yake ni “Mtumishi wa Yehova.” Mambo pekee yanayojulikana kuhusu nabii huyu ni haya yaliyoandikwa katika kitabu hiki chenye unabii wake. Obadia alitoa unabii kuhusu hukumu ya Mungu dhidi ya taifa la Edomu, kukomeshwa na kuangamizwa kwalo lisiwepo tena ulimwenguni. Waedomu, ambao walikuwa uzao wa Esau, walijivunia usalama katika ngome zao zilizokuwa kwenye Mlima Seiri, kusini mwa Bahari ya Chumvi. Waliwatazama watu wa Yuda walipopatwa na mikasa mikononi mwa wavamizi bila kuwasaidia. Mwanzoni mwa karne ya tisa Waedomu wenyewe walishiriki zaidi ya mara nne kuiteka nyara Yerusalemu.Wazo Kuu

Obadia alitangaza hukumu ya Mungu dhidi ya Waedomu na akatabiri kuangamizwa kwao na kufutwa kwa kumbukumbu lao katika uso wa dunia. Wale wanaopigana na watu walioitwa na Mungu, yeye hupigana nao na kufuta kumbukumbu lao duniani wasipotubu.Mwandishi

Obadia.Kusudi

Kuonyesha kwamba Mungu anawahukumu wale wanaowadhuru watu wake.Mambo Muhimu

Hukumu la Mungu na kuangamizwa kwa taifa la Waedomu.Mahali

Yerusalemu.Tarehe

Kati ya 605-586 K.K.Wahusika Wakuu

Waedomu.Mgawanyo

  • • Maangamizi ya Edomu (1:1-14)
  • • Kurejeshwa kwa Israeli (1:15-21).

Obadiah

1Maono ya Obadia.

Hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi kuhusu Edomu:

Tumesikia ujumbe kutoka kwa BWANA:
Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema,
“Inukeni, na twendeni tukapigane vita dhidi ya Edomu.”
2“Angalieni, nitawafanya wadogo miongoni mwa mataifa,
mtadharauliwa kabisa.
3Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,
wewe unayeishi kwenye nyufa za miamba
na kufanya makao yako juu,
wewe unayejiambia mwenyewe,
‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’
4Ingawa unapaa juu kama tai
na kufanya kiota chako kati ya nyota,
kutoka huko nitakushusha chini,”
asema BWANA.

5“Ikiwa wevi wangekuja kwako,
ikiwa wanyang'anyi wangekujia usiku:
Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yangekuwa yanakungojea:
je, si wangeiba tu kiasi kile wanachotaka?
Kama wachuma zabibu wangekuja kwako,
je, wasingebakiza zabibu chache?
6Lakini tazama ni jinsi gani Esau atatekwa,
hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara!
7Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani,
rafiki zako watakudanganya na kukushinda,
wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego
lakini hutaweza kuugundua.
8“Katika siku hiyo,” asema BWANA,
“je, sitaangamiza watu wenye hekima wa Edomu,
watu wenye ufahamu katika milima ya Esau?
9Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu,
kila mmoja katika milima ya Esau
ataangushwa chini kwa kuchinjwa.
10Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo,
aibu itakufunika;
utaangamizwa milele.
11Siku ile ulisimama mbali ukiangalia
wakati wageni walipojichukulia utajiri wake
na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake
wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu,
ulikuwa kama mmoja wao.
12Usingemdharau ndugu yako
katika siku ya msiba wake,
wala kufurahia juu ya watu wa Yuda
katika siku ya maangamizi yao,
wala kujigamba sana
katika siku ya taabu yao.
13Usingeingia katika malango ya watu wangu
katika siku ya maafa yao,
wala kuwadharau katika janga lao
katika siku ya maafa yao,
wala kunyang'anya mali zao
katika siku ya maafa yao.
14Usingengoja kwenye njia panda
na kuwaua wakimbizi wao,
wala kuwatoa watu wake waliosalia
katika siku ya shida yao.
15“Siku ya BWANA i karibu
kwa mataifa yote.
Kama ulivyofanya, nawe utafanyiwa vivyo hivyo,
matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako.
16Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu,
vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo,
watakunywa na kunywa,
nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo.
17Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwepo
na wale watakaookoka;
nao utakuwa mtakatifu,
nayo nyumba ya Yakobo
itamiliki urithi wake.
18Nyumba ya Yakobo itakuwa moto,
na nyumba ya Yosefu itakuwa mwali wa moto;
nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu,
nao wataiwasha moto na kuiteketeza.
Hakutakuwa na watakaosalimika
kutoka katika nyumba ya Esau.”
BWANA amesema.

19Watu kutoka nchi ya Negebu
wataikalia milima ya Esau,
na watu kutoka mitelemko ya vilima
watamiliki nchi ya Wafilisti.
Watayakalia mashamba ya Efraimu na Samaria,
naye Benyamini atamiliki Gileadi.
20Kundi la Waisraeli walioko uhamishoni Kanaani
watarudi na kumiliki nchi mpaka Sarepta.
Walioko uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu
watamiliki miji ya Negebu.
21Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni
kutawala milima ya Esau.
Nao ufalme utakuwa wa BWANA.


Copyright information for Neno