Philippians 2

Kuiga Unyenyekevu Wa Kristo

1Kama kukiwa na jambo lo lote la kutia moyo, kukiwako faraja yo yote katika upendo, kukiwa na ushirika wo wote katika Roho, kukiwa na wema wo wote na huruma, 2basi ikamilisheni furaha yangu kwa kuwa na nia kama hiyo, mkiwa na upendo huo huo, wenye roho moja na kusudi moja. 3Msitende jambo lo lote kwa nia ya kujitukuza, bali kwa unyenyekevu, kila mtu akimhesabu mwingine bora kuliko nafsi yake. 4Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine.

5Iweni na nia ile ile aliyokuwa nayo Kristo Yesu: 6Yeye, ingawa alikuwa na asili ya Mungu hasa,
hakuona kule kuwa sawa na Mungu
ni kitu cha kushikilia,
7bali alijifanya si kitu,
akajifanya sawa hasa na mtumwa,
akazaliwa katika umbo la mwanadamu.
8Naye akiwa na umbo la mwanadamu,
alijinyenyekeza, akatii hata mauti:
naam, mauti ya msalaba!
9Kwa hiyo, Mungu alimtukuza juu sana
na kumpa Jina lililo kuu kuliko kila jina,
10ili kwa Jina la Yesu, kila goti lipigwe,
la vitu vya mbinguni, vya duniani
na vya chini ya nchi,
11na kila ulimi ukiri ya kwamba
YESU KRISTO NI BWANA,
kwa utukufu wa Mungu Baba.


Ng'aeni Kama Mianga Katika Ulimwengu

12Kwa hiyo, wapenzi wangu, kama vile ambavyo mmekuwa mkitii siku zote, si tu wakati nikiwa pamoja nanyi, bali sasa zaidi sana nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu kwa kuogopa na kutetemeka, 13kwa maana Mungu ndiye atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu kwa kulitimiza kusudi lake jema.

14Fanyeni mambo yote bila kunung'unika wala kushindana, 15ili msiwe na lawama wala hatia, bali mwe wana wa Mungu wasio na kasoro katika kizazi chenye ukaidi na kilichopotoka, ambacho ndani yake ninyi mnang'aa kama mianga ulimwenguni. 16Mkilishika neno la uzima, ili nipate kuona fahari siku ya Kristo kwamba sikupiga mbio wala kujitaabisha bure. 17Lakini hata kama nikimiminwa kama sadaka ya kinywaji kwenye dhabihu na huduma itokayo katika imani yenu, mimi ninafurahi na kushangilia pamoja nanyi nyote. 18Vivyo hivyo, ninyi nanyi imewapasa kufurahi na kushangilia pamoja nami.

Paulo Amsifu Timotheo

19Natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo hivi karibuni aje kwenu, ili nipate kufarijika moyo nitakapopata habari zenu. 20Sina mtu mwingine kama yeye ambaye ataangalia hali yenu kwa halisi. 21Kwa maana kila mmoja anajishughulisha zaidi na mambo yake mwenyewe wala si yale ya Yesu Kristo. 22Lakini ninyi wenyewe mnajua jinsi Timotheo alivyojithibitisha mwenyewe, kwa maana amefanya kazi ya Injili pamoja nami kama vile mwana kwa baba yake. 23Kwa hiyo, ninatumaini kumtuma kwenu upesi mara nitakapojua mambo yangu yatakavyokuwa. 24Nami mwenyewe ninatumaini katika Bwana kwamba nitakuja kwenu hivi karibuni.

Paulo Amsifu Epafrodito

25Lakini nadhani ni muhimu kumtuma tena kwenu Epafrodito, ndugu yangu na mtenda kazi pamoja nami, aliye askari mwenzangu, ambaye pia ni mjumbe wenu mliyemtuma ili ashughulike na mahitaji yangu. 26Kwa maana amekuwa akiwaonea sana shauku ninyi nyote, akiwa na wasiwasi kwa kuwa mlisikia kwamba alikuwa mgonjwa. 27Kweli alikuwa mgonjwa, tena karibu ya kufa. Lakini Mungu alimhurumia, wala si yeye tu, bali hata na mimi alinihurumia, nisipatwe na huzuni juu ya huzuni. 28Kwa hiyo mimi ninafanya bidii kumtuma kwenu ili mtakapomwona kwa mara nyingine, mpate kufurahi, nami wasiwasi wangu upungue. 29Kwa hiyo mpokeeni katika Bwana kwa furaha kubwa, nanyi wapeni heshima watu kama hawa, 30kwa sababu alikaribia kufa kwa ajili ya kazi ya Kristo, akihatarisha maisha yake ili aweze kunipa msaada ambao ninyi hamkuweza kunipa.

Copyright information for Neno