Philippians 3

Hakuna Tumaini Katika Mwili

1Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana! Mimi kuwaandikia mambo yale yale hakuniudhi, kwa maana ni kinga kwa ajili yenu.

2Jihadharini na mbwa, wale watenda maovu, jihadharini na wale wajikatao miili yao, wasemao ili kuokoka ni lazima kutahiriwa. 3Kwa maana sisi ndio tulio tohara, sisi tumwabuduo Mungu katika Roho, tunaona fahari katika Kristo Yesu, ambao hatuweki tumaini letu katika mwili, 4ingawa mimi mwenyewe ninazo sababu za kuutumainia mwili.

Kama mtu ye yote akidhani anazo sababu za kuutumainia mwili, mimi zaidi.
5Nilitahiriwa siku ya nane, mimi ni Mwisraeli wa kabila la Benyamini, Mwebrania wa Waebrania. Kwa habari ya sheria, ni Farisayo, 6kwa habari ya juhudi, nilikuwa nalitesa kanisa, kuhusu haki ipatikanayo kwa sheria, mimi nilikuwa sina hatia.

7Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, sasa nayahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. 8Zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara tupu nikiyalinganisha na faida kubwa ipitayo kiasi ya kumjua Kristo Yesu Bwana wangu, ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote, nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo, 9nami nionekane mbele zake nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu kwa njia ya imani. 10Nataka nimjue Kristo na uweza wa kufufuka kwake na ushirika wa mateso yake, ili nifanane naye katika mauti yake, 11ili kwa njia yo yote niweze kufikia ufufuo wa wafu.

Kukaza Mwendo Ili Kufikia Lengo

12Si kwamba nimekwisha kufikia, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha! Bali nakaza mwendo ili nipate kile ambacho kwa ajili yake, nimeshikwa na Kristo Yesu. 13Ndugu zangu, sijihesabu kuwa nimekwisha kushika. Lakini ninafanya jambo moja: Ninasahau mambo yale yaliyopita, nakaza mwendo kufikia yale yaliyo mbele. 14Nakaza mwendo nifikie ile alama ya ushindi iliyowekwa ili nipate tuzo ya mwito mkuu wa Mungu ambao nimeitiwa huko juu mbinguni katika Kristo Yesu.

15Hivyo sisi sote tuliokuwa kiroho tuwaze jambo hili, hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu ataliweka wazi hilo nalo. 16Lakini na tushike sana lile ambalo tumekwisha kulifikia.

17Ndugu zangu, kwa pamoja fuateni mfano wangu na kuwatazama wale wanaofuata kielelezo tulichowawekea. 18Kwa maana, kama nilivyokwisha kuwaambia mara nyingi kabla, nami sasa nasema tena hata kwa machozi, watu wengi wanaishi kama adui wa msalaba wa Kristo. 19Mwisho wa watu hao ni uangamivu, Mungu wao ni tumbo na utukufu wao ni aibu na mawazo yao yamo katika mambo ya dunia. 20Lakini uenyeji wetu uko mbinguni. Nasi tunamngoja kwa shauku Mwokozi kutoka huko, yaani, Bwana Yesu Kristo, 21atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, ili upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote chini yake.

Copyright information for Neno