Proverbs 10

Mithali Za Solomoni

1Mithali za Solomoni: Mwana mwenye hekima
huleta furaha kwa baba yake,
lakini mwana mpumbavu
huleta huzuni kwa mama yake.
2Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,
lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.
3BWANA hawaachi waadilifu kukaa njaa,
lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.
4Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini
lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.
5Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi
ni mwana mwenye hekima,
lakini yeye alalaye wakati wa mavuno
ni mwana mwenye kuaibisha.
6Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
7Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka,
lakini jina la mwovu litaoza.
8Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo,
lakini mpumbavu apayukaye huangamia.
9Mtu mwadilifu hutembea salama,
lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagundulika.
10Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni,
naye mpumbavu apayukaye huangamia.
11Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,
lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.
12Chuki huchochea faraka,
lakini upendo husitiri mabaya yote.
13Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua,
lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.
14Wenye hekima huhifadhi maarifa,
bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.
15Mali ya tajiri ni mji wao wenye ngome,
bali ufukara ni maangamizi ya maskini.
16Ujira wa wenye haki huwaletea uzima,
lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.
17Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima,
lakini ye yote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.
18Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,
na ye yote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.
19Wakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani,
lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.
20Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora,
bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.
21Midomo ya mwenye haki hulisha wengi,
lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.
22Baraka ya BWANA hutajirisha,
wala haichanganyi huzuni.
23Mpumbavu hufurahia tabia mbaya,
lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.
24Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata,
kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.
25Tufani inapopita, waovu hutoweka,
lakini wenye haki husimama imara milele.
26Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,
ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.
27Kumcha BWANA huongeza urefu wa maisha,
lakini miaka ya mwovu inafupishwa.
28Tarajio la mwenye haki ni furaha,
bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.
29Njia ya BWANA ni kimbilio kwa wenye haki,
lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.
30Kamwe wenye haki hawataondolewa,
bali waovu hawatasalia katika nchi.
31Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima,
bali ulimi wa upotovu utakatwa.
32Midomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa,
bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.


Copyright information for Neno