Proverbs 2

Faida Za Hekima

Mwanangu, kama utayakubali maneno yangu
na kuyaweka akiba maagizo yangu ndani mwako,
kutega sikio lako kwenye hekima
na kuweka moyo wako katika ufahamu,
na kama ukiita busara
na kuita kwa sauti ufahamu,
na kama utaitafuta kama fedha
na kuitafuta sana kama hazina iliyofichwa,
ndipo utakapoelewa kumcha BWANA
na kupata maarifa ya Mungu.
Kwa maana BWANA hutoa hekima,
na kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu.
Huifadhi ushindi kwa ajili ya mwadilifu,
yeye ni ngao kwa wale wasio na lawama,
kwa kuwa hulinda mwenendo wa mwenye haki
na kuhifadhi njia ya waaminifu wake.
Ndipo utafahamu lipi lililo kweli na haki
na sawa, katika kila njia nzuri.
10 Kwa maana hekima itaingia moyoni mwako,
nayo maarifa yataifurahisha nafsi yako.
11 Busara itakuhifadhi
na ufahamu utakulinda.
12 Hekima itakuokoa kutoka katika njia za waovu,
kutoka watu ambao maneno yao yamepotoka,
13 wale waachao mapito yaliyonyooka
wakatembea katika njia za giza,
14 wale wapendao kutenda mabaya
na kufurahia upotovu wa ubaya,
15 ambao mapito yao yamepotoka
na ambao ni wapotovu katika njia zao.
16 Itakuokoa pia kutokana na mwanamke kahaba,
kutokana na mke aliyepotoka mwenye maneno
ya kushawishi kutenda ubaya,
17 aliyemwacha mwenzi wa ujana wake
na kupuuza agano alilofanya mbele ya Mungu.
18 Kwa maana nyumba yake huelekea kwenye kifo
na mapito yake kwenye roho za waliokufa.
19 Hakuna ye yote aendaye kwake akarudi,
au kufikia mapito ya uzima.
20 Hivyo utatembea katika njia za watu wema
na kushikamana na mapito ya wenye haki.
21 Kwa maana wanyofu wataishi katika nchi,
nao wasio na lawama watabakia ndani yake,
22 bali waovu watakatiliwa mbali kutoka katika nchi,
nao wasio waaminifu watang'olewa kutoka humo.
Copyright information for Neno