Proverbs 23

1Uketipo kula chakula na mtawala,
angalia vyema kile kilicho mbele yako,
2na utie kisu kooni mwako
kama ukiwa mlafi.
3Usitamani vyakula vyake vitamu
kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.
4Usijitaabishe ili kuupata utajiri,
uwe na hekima kuonyesha kujizuia.
5Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka,
huwa kama umepata mabawa ghafula,
ukaruka na kutoweka angani kama tai.
6Usile chakula cha mtu mchoyo,
usitamani vyakula vyake vitamu,
7kwa maana yeye ni aina ya mtu
ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama.
Anakuambia, “Kula na kunywa,”
lakini moyo wake hauko pamoja nawe.
8Utatapika kile kidogo ulichokula,
nawe utakuwa umepoteza bure
maneno yako ya kumsifu.
9Usizungumze na mpumbavu,
kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.
10Usiondoe jiwe la mpaka wa zamani
wala kujiingiza kwenye mashamba ya yatima,
11kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu,
atalichukua shauri lao dhidi yako.
12Elekeza moyo wako kwenye mafundisho
na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
13Usimnyime mtoto adhabu,
kwa maana ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.
14Mwadhibu kwa fimbo
na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini
23.14 Mautini maana yake ni Kuzimu
.
15Mwanangu, kama moyo wako una hekima,
basi moyo wangu utafurahi,
16utu wangu wa ndani utafurahi,
wakati midomo yako
itakapozungumza lililo sawa.
17Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi,
bali kila mara uwe na bidii katika kumcha BWANA.
18Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako,
nalo taraja lako halitakatiliwa mbali.
19Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima,
weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.
20Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo,
au wale walao nyama kwa pupa,
21kwa maana walevi na walafi huwa maskini,
nako kusinzia huwavika matambara.
22Msikilize baba yako, aliyekuzaa,
wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
23Nunua kweli wala usiiuze,
pata hekima, adabu na ufahamu.
24Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa,
naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
25Baba yako na mama yako na wafurahi,
mama aliyekuzaa na ashangilie!
26Mwanangu, nipe moyo wako,
macho yako na yafuate njia zangu,
27kwa maana kahaba ni shimo refu
na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.
28Kama mnyang'anyi, hungojea akivizia,
naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.
29Ni nani mwenye ole?
Ni nani mwenye huzuni?
Ni nani mwenye ugomvi?
Ni nani mwenye malalamiko?
Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?
Ni nani mwenye macho mekundu?
30Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo,
hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.
31Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu,
wakati unapometameta kwenye bilauri,
wakati ushukapo taratibu!
32Mwisho huuma kama nyoka
na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.
33Macho yako yataona mambo mageni
na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.
34Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari,
alalaye juu ya kamba ya merikebu.
35Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia!
Wamenichapa, lakini sisikii!
Nitaamka lini
ili nikanywe tena?”
Copyright information for Neno