Proverbs 27

Usijisifu kwa ajili ya kesho,
kwa kuwa hujui ni nini kitakachozaliwa kwa siku moja.
Mwache mwingine akusifu,
wala si kinywa chako mwenyewe;
mtu mwingine afanye hivyo
na si midomo yako mwenyewe.
Jiwe ni zito na mchanga ni mzigo,
lakini kukasirishwa na mpumbavu ni kuzito
zaidi kuliko hivyo vyote viwili.
Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika,
lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?
Afadhali karipio la wazi
kuliko upendo uliofichika.
Majeraha kutoka kwa rafiki yaonyesha uaminifu,
bali busu la adui ni udanganyifu.
Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali,
bali kwa mwenye njaa
hata kile kilicho kichungu
kwake ni kitamu.
Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake,
ndivyo alivyo mtu atangatangaye
mbali na nyumbani mwake.
Manukato na uvumba huleta furaha moyoni,
nao uzuri wa rafiki huchipuka
kutoka kwenye ushauri wake wa uaminifu.
10 Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako,
tena usiende nyumbani mwa ndugu yako
wakati umepatwa na maafa.
bora jirani wa karibu
kuliko ndugu aliye mbali.
11 Mwanangu, uwe na hekima,
nawe ulete furaha moyoni mwangu,
ndipo nitakapoweza kumjibu ye yote
anitendaye kwa dharau.
12 Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha,
bali mjinga huendelea mbele nayo ikamtesa.
13 Chukua vazi la yule awekaye dhamana
kwa ajili ya mgeni;
lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo
kwa ajili ya mwanamke mgeni.
14 Kama mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu
asubuhi na mapema,
itahesabiwa kama ni laana.
15 Mke mgomvi ni kama
matone yasiyokoma ya siku ya mvua.
16 Kumzuia yeye ni kama kuuzuia upepo
au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono.
17 Kama vile chuma kinoavyo chuma,
ndivyo mtu amnoavyo mwenzake.
18 Yeye atunzaye mtini atakula tunda lake,
naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa.
19 Kama uso uonekanavyo kwenye maji,
ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonyesha alivyo.
20 Kuzimu na uharibifu havishibi
kadhalika macho ya mwanadamu.
21 Kalibu ni kwa ajili ya fedha
na tanuru kwa ajili ya dhahabu,
bali mtu hupimwa kwa sifa azipokeazo.
22 Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu,
ukimtwanga kama nafaka kwa mchi,
hutauondoa upumbavu wake.
23 Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako
ya kondoo na mbuzi,
angalia kwa bidii ng'ombe zako.
24 Kwa kuwa utajiri haudumu milele,
nayo taji haidumu vizazi vyote.
25 Wakati majani makavu yameondolewa
na mapya yamechipua,
nayo majani toka milimani yamekusanywa,
26 wana-kondoo watakupatia mavazi
na mbuzi thamani ya shamba.
27 Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi
kukulisha wewe na jamaa yako,
na kuwalisha watumishi wako wa kike.
Copyright information for Neno