Proverbs 29

1Mtu anayeendelea kuwa na shingo ngumu baada ya maonyo mengi,
ataangamia ghafula, wala hapati dawa.
2Wenye haki wanapostawi, watu hufurahi;
waovu watawalapo, watu hulia kwa huzuni.
3Mtu apendaye hekima huleta furaha kwa baba yake,
bali aambatanaye na kahaba hutapanya mali yake.
4Kwa haki mfalme huipa nchi uthabiti,
bali mfalme aliye na tamaa ya rushwa huiangamiza.
5Ye yote amsifuye jirani yake isivyostahili,
anautandaza wavu kuitega miguu yake.
6Mtu mbaya hutegwa na dhambi yake mwenyewe
bali mwenye haki huweza kuimba na kufurahi.
7Mwenye haki hujali haki kwa ajili ya maskini,
bali mwovu hajishughulishi na hilo.
8Wenye mzaha huuchochea mji,
bali watu wenye hekima hugeuzia mbali hasira.
9Kama mwenye hekima akienda mahakamani na mpumbavu,
mpumbavu hukasirika na kudhihaki, wala hakuna amani.
10Watu wamwagao damu humchukia mtu mwadilifu
na hutafuta kumwua mtu mnyofu.
11Mpumbavu huonyesha hasira yake yote,
bali mwenye hekima hujizuia.
12Kama mtawala akisikiliza uongo,
maafisa wake wote huwa waovu.
13Mtu maskini na mtu anayeonea wanafanana kwa jambo hili:
BWANA hutia nuru macho yao wote wawili.
14Kama mfalme akiwaamua maskini kwa haki,
kiti chake cha enzi kitakuwa thabiti siku zote.
15Fimbo ya maonyo hutia hekima,
bali mtoto aliyeachiwa bila maonyo
humwaibisha mama yake.
16Wakati waovu wanapostawi,
pia dhambi vivyo hivyo,
lakini wenye haki wataliona anguko lao.
17Mrudi mwanao, naye atakupa amani,
atakufurahisha nafsi yako.
18Mahali pasipo na maono, watu huangamia,
bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
19Mtumishi hawezi kuonywa kwa maneno matupu,
ajapoelewa, hataitikia.
20Je, unamwona mtu azungumzaye kwa haraka?
Kuna matumaini zaidi kwa mpumbavu kuliko yeye.
21Kama mtu akimdekeza mtumishi wake tangu ujanani,
atamletea sikitiko mwishoni.
22Mtu mwenye hasira huchochea ugomvi,
naye mtu mwenye hasira ya haraka
hutenda dhambi nyingi.
23Kiburi cha mtu humshusha,
bali mtu mwenye roho ya unyenyekevu
hupata heshima.
24Anayekubaliana na mwizi ni adui wa nafsi yake mwenyewe;
huapishwa lakini hathubutu kushuhudia.
25Kuwaogopa watu huwa ni mtego,
bali ye yote amtumainiaye BWANA atakuwa salama.
26Watu wengi hutafuta kusikilizwa na mtawala,
bali mtu hupata haki kutoka kwa BWANA.
27Mwenye haki huwachukia sana wasio waaminifu;
waovu huwachukia sana wenye haki.
Copyright information for Neno