Proverbs 3

Faida Nyingine Za Hekima

1Mwanangu, usisahau mafundisho yangu,
bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
2kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako
na kukuletea mafanikio.
3Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe;
vifunge shingoni mwako,
viandike katika ubao wa moyo wako.
4Ndipo utapata kibali na jina zuri
mbele za Mungu na mwanadamu.
5Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote
wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6katika njia zako zote mkiri yeye,
naye atayanyosha mapito yako.
7Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe,
mche BWANA ukajiepushe na uovu.
8Hii itakuletea afya mwilini mwako,
na mafuta kwenye mifupa yako.
9Mheshimu BWANA kwa mali zako na
kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika,
viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
11Mwanangu, usidharau marudi ya BWANA
na usichukie kukaripiwa naye,
12kwa sababu BWANA huwarudi wale awapendao,
kama vile baba afanyavyo
kwa mwana apendezwaye naye.
13Heri mtu yule aonaye hekima,
mtu yule apataye ufahamu,
14kwa maana hekima ana faida kuliko fedha
na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
15Hekima ana thamani kuliko marijani,
hakuna cho chote unachokitamani
kinachoweza kulinganishwa naye.
16Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume,
katika mkono wake wa kushoto
kuna utajiri na heshima.
17Njia zake zinapendeza,
mapito yake yote ni amani.
18Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia;
wale wamshikao watabarikiwa.
19Kwa hekima BWANA aliiweka misingi ya dunia,
kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
20kwa maarifa yake vilindi viligawanywa,
nayo mawingu yanadondosha umande.
21Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara,
usiache vitoke machoni pako;
22ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako
na pambo la neema shingoni mwako.
23Kisha utaenda katika njia yako salama,
wala mguu wako hautajikwaa;
24ulalapo, hautaogopa;
ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.
25Usiogope maafa ya ghafula
au maangamizi yanayowapata waovu,
26kwa kuwa BWANA atakuwa tumaini lako
na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
27Usizuie wema kwa wale wanaostahili
ikiwa katika uwezo wako kutenda.
28Usimwambie jirani yako,
“Njoo baadaye, nitakupa kesho,”
wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
29Usifanye hila ya kumdhuru jirani yako,
ambaye anaishi karibu na wewe akikuamini.
30Usimshtaki mtu bila sababu,
wakati hajakutenda dhara lo lote.
31Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri
wala kuchagua njia yake iwayo yote,
32kwa kuwa BWANA humchukia mtu mpotovu,
lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
33Laana ya BWANA i juu ya nyumba ya mwovu,
lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
34Huwadhihaki wale wanaodhihaki kwa kiburi
lakini huwapa neema wanyenyekevu.
35Wenye hekima hurithi heshima,
bali huwaaibisha wapumbavu.
Copyright information for Neno