Proverbs 6

Maonyo Dhidi Ya Upumbavu

Mwanangu, kama umekuwa mdhamini wa jirani yako,
ikiwa umeshika mikono kwa kuweka ahadi
kwa ajili ya mwingine,
kama umetegwa na ulichosema,
umenaswa kwa maneno ya kinywa chako,
basi fanya hivi mwanangu, ili ujiweke huru,
kwa kuwa umeanguka mikononi mwa jirani yako:
Nenda ukajinyenyekeshe kwake,
msihi jirani yako!
Usiruhusu usingizi machoni pako,
usiruhusu kope zako zisinzie.
Jiweke huru, kama swala mkononi mwa mwindaji,
kama ndege kutoka kwenye mtego wa mwindaji.
Ewe mvivu, mwendee mchwa,
zitafakari njia zake ukapate hekima!
Kwa maana yeye hana msimamizi,
wala mwangalizi, au mtawala,
lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi
na hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.
Ewe mvivu, utalala hata lini?
Utaamka lini kutoka katika usingizi wako?
10 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo,
bado kukunja mikono upate usingizi!
11 Hivyo umaskini wako huja kama mnyang'anyi
na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha.
12 Mtu mbaya sana na mlaghai,
ambaye huzungukazunguka
na maneno ya upotovu,
13 ambaye anakonyeza kwa jicho lake,
anayetoa ishara kwa miguu yake
na kuashiria kwa vidole vyake,
14 ambaye hupanga ubaya
kwa udanganyifu moyoni mwake:
daima huchochea fitina.
15 Kwa hiyo maafa yatamkumba ghafula;
ataangamizwa mara, pasipo msaada.
16 Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA,
naam, viko saba vilivyo chukizo kwake:
17 macho ya kiburi,
ulimi udanganyao,
mikono imwagayo damu isiyo na hatia,
18 moyo ule uwazao mipango miovu,
miguu ile iliyo myepesi kukimbilia uovu,
19 shahidi wa uongo ambaye humwaga uongo
na mtu ambaye huchochea fitina kati ya ndugu.

Onyo Dhidi Ya Uasherati

20 Mwanangu, zishike amri za baba yako,
wala usiyaache mafundisho ya mama yako.
21 Yafunge katika moyo wako daima,
yakaze kuizunguka shingo yako.
22 Wakati utembeapo, yatakuongoza,
wakati ulalapo, yatakulinda,
wakati uamkapo, yatazungumza nawe.
23 Kwa maana amri hizi ni taa,
mafundisho haya ni mwanga
na maonyo ya maadili ni njia ya uzima,
24 yakikulinda na mwanamke aliyepotoka,
kutokana na maneno laini ya mwanamke aliyepotoka.
25 Moyo wako usitamani uzuri wake
wala macho yake yasikuteke,
26 kwa maana kahaba atakufanya uwe maskini
hata ukose kipande cha mkate
naye mwanamke mzinzi huwinda maisha yako hasa.
27 Je, mtu aweza kuchotea moto kwenye paja lake
bila nguo zake kuungua?
28 Je, mtu aweza kutembea juu ya makaa ya moto yanayowaka
bila miguu yake kuungua?
29 Ndivyo alivyo mtu alalaye na mke wa mwanaume mwingine;
hakuna ye yote amgusaye huyo mwanamke ambaye hataadhibiwa.
30 Watu hawamdharau mwizi kama akiiba
kukidhi njaa yake wakati ana njaa.
31 Pamoja na hayo, kama akikamatwa,
lazima alipe mara saba,
ingawa inamgharimu utajiri wote wa nyumba yake.
32 Lakini mwanaume aziniye na mwanamke hana akili kabisa;
ye yote afanyaye hivyo hujiangamiza mwenyewe.
33 Mapigo na aibu ni fungu lake
na aibu yake haitafutika kamwe;
34 kwa maana wivu huamsha ghadhabu ya mume,
naye hataonyesha huruma alipizapo kisasi.
35 Hatakubali fidia yo yote;
atakataa malipo hata yakiwa makubwa kiasi gani.
Copyright information for Neno