Proverbs 8

Wito Wa Hekima

1Je, hekima haiti?
Je, ufahamu hapazi sauti?
2Juu ya miinuko karibu na njia,
penye njia panda, ndipo asimamapo,
3kando ya malango yaelekeayo mjini,
kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:
4“Ni ninyi wanaume, ninaowaita,
ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.
5Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili,
ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.
6Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema,
ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.
7Kinywa changu husema lililo kweli,
kwa maana midomo yangu huchukia uovu.
8Maneno yote ya kinywa changu ni haki,
hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi.
9Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi,
hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.
10Chagua mafundisho yangu badala ya fedha,
maarifa badala ya dhahabu safi,
11kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani
na hakuna cho chote unachohitaji kinacholingana naye.
12“Mimi hekima, nakaa pamoja na busara,
ninamiliki maarifa na busara.
13Kumcha BWANA ni kuchukia uovu,
ninachukia kiburi na majivuno,
tabia mbaya na mazungumzo potovu.
14Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu,
nina ufahamu na nina nguvu.
15Kwa msaada wangu wafalme hutawala
na watawala hutunga sheria zilizo za haki,
16kwa msaada wangu wakuu hutawala,
na wenye vyeo wote watawalao dunia.
17Nawapenda wale wanipendao,
na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18Utajiri na heshima viko kwangu,
utajiri udumuo na mafanikio.
19Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi,
kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.
20Natembea katika njia ya unyofu
katika mapito ya haki,
21nawapa utajiri wale wanipendao
na kuzijaza hazina zao.
22“BWANA aliniumba mwanzoni mwa kazi yake,
kabla ya matendo yake ya zamani;
23niliteuliwa tangu milele,
tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.
24Wakati hazijakuwapo bahari, nilikwishazaliwa,
wakati hazijakuwapo chemchemi zilizojaa maji,
25kabla milima haijawekwa mahali pake,
kabla vilima havijakuwapo, nilikwishazaliwa,
26kabla hajaumba dunia wala mashamba yake
au vumbi lo lote la dunia.
27Nilikuwapo alipoziweka mbingu mahali pake,
wakati alipochora mstari wa upeo wa macho
juu ya uso wa kilindi,
28wakati alipoweka mawingu juu
na kuziweka imara chemchemi za bahari,
29wakati alipoiwekea bahari mpaka wake
ili maji yasivunje agizo lake,
na wakati alipoweka misingi ya dunia.
30Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake.
Nilijazwa na furaha siku baada ya siku,
nikifurahi daima mbele zake,
31nikifurahi katika dunia yake yote
nami nikiwafurahia wanadamu.
32“Basi sasa wanangu, nisikilizeni;
heri wale wanaozishika njia zangu.
33Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima;
msiyapuuze.
34Heri mtu yule anisikilizae mimi,
akisubiri siku zote malangoni mwangu,
akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.
35Kwa maana ye yote anipatae mimi amepata uzima
na kujipatia kibali kutoka kwa BWANA.
36Lakini ye yote ashindwaye kunipata
hujiumiza mwenyewe;
na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”
Copyright information for Neno