Proverbs 28

1Mtu mwovu hukimbia ingawa hakuna ye yote anayemfukuza,
bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
2Wakati nchi inapokuwa na uasi, inakuwa na viongozi wengi,
bali mwenye ufahamu na maarifa hudumisha utaratibu.
3Mtu maskini amwoneaye yeye aliye maskini zaidi
ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza mazao.
4Wale waiachao sheria huwasifu waovu,
bali wale waishikao sheria huwapinga.
5Watu wabaya hawaelewi haki,
bali wale wamtafutao BWANA wanaielewa kikamilifu.
6Afadhali maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama
kuliko tajiri ambaye njia zake ni potovu.
7Yeye ashikaye sheria ni mwana mwenye hekima,
bali rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.
8Yeye aongezaye utajiri wake kwa riba kubwa mno
hukusanya kwa ajili ya mwingine,
ambaye atamhurumia maskini.
9Kama mtu ye yote akikataa kusikia sheria,
hata maombi yake ni chukizo.
10Yeye ambaye humwongoza mwenye haki kwenye mapito mabaya,
ataanguka kwenye mtego wake mwenyewe,
bali wasio na lawama watapokea urithi mwema.
11Mtu tajiri anaweza kuwa na hekima machoni pake mwenyewe,
bali mtu maskini mwenye ufahamu atamfichua.
12Mwenye haki ashindapo, kuna furaha kubwa,
bali mwovu atawalapo, watu hujificha.
13Yeye afichaye dhambi zake hatafanikiwa,
bali ye yote aziungamaye na kuziacha hupata rehema.
14Amebarikiwa mtu ambaye siku zote humcha BWANA,
bali yeye afanyaye moyo wake kuwa mgumu
huangukia kwenye taabu.
15Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye,
divyo alivyo mtu mwovu atawalaye wanyonge.
16Mtawala dhalimu hana akili,
bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu
atafurahia maisha marefu.
17Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua
atakuwa mtoro mpaka kufa;
mtu ye yote na asimsaidie.
18Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama
hulindwa salama,
bali yeye ambaye njia zake ni potovu
ataanguka ghafula.
19Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,
bali afuataye mambo ya upuzi
atakuwa na umaskini wa kumtosha.
20Mtu mwaminifu atabarikiwa sana,
bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka
hataacha kuadhibiwa.
21Kuonyesha upendeleo si vizuri,
hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate.
22Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri,
naye hana habari kuwa umaskini unamngojea.
23Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi,
kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili.
24Yeye amwibiaye babaye au mamaye
na kusema, “Si kosa,”
yeye ni mwenzi wa yule aharibuye.
25Mtu mwenye tamaa huchochea fitina,
bali yule amtegemeaye BWANA atafanikiwa.
26Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu,
bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama.
27Yeye ampaye maskini
hatapungukiwa na kitu cho chote,
bali yeye awafumbiaye maskini macho
hupata laana nyingi.
28Wakati mwovu atawalapo,
watu huenda mafichoni,
bali mwovu anapoangamia,
wenye haki hufanikiwa.
Copyright information for Neno