Psalms 10

10:0 Zaburi hii ikiunganishwa na ya 9 zimetungwa kila beti likianzia na herufi ya alfabeti ya Kiebrania zikifuatana tangu Aleph (A) hadi Taw (T); zote ni 22

Sala Kwa Ajili Ya Haki

1Kwa nini, Ee BWANA, unasimama mbali?
Kwa nini unajificha wakati wa shida?
2Katika kiburi chake mtu mwovu humtesa mtu aliye maskini,
waovu na wanaswe katika hila wanazozitunga.
3Hujivunia tamaa za moyo wake;
humbariki mlafi na kumtukana BWANA.
4Katika kiburi chake mtu mwovu hamtafuti Mungu,
katika mawazo yake yote
hakuna nafasi ya Mungu.
5Njia zake daima hufanikiwa;
hujivuna na amri zako ziko mbali naye,
huwacheka kwa dharau adui zake wote.
6Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa,
daima nitakuwa na furaha,
kamwe sitakuwa na shida.”
7Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho,
shida na ubaya viko chini ya ulimi wake.
8Huvizia karibu na vijiji;
kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia,
akivizia wapitaji.
9Huvizia kama simba aliye mawindoni;
huvizia kumkamata mnyonge,
huwakamata wanyonge na kuwaburuza
katika wavu wake.
10Mateka wake hupondwa, huzimia;
wanaanguka katika nguvu zake.
11Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau,
huficha uso wake na haoni kabisa.”
12Inuka BWANA! Inua mkono wako, Ee Mungu.
Usiwasahau wanyonge.
13Kwa nini mtu mwovu anamtukana Mungu?
Kwa nini anajiambia mwenyewe,
“Hataniita nitoe hesabu?”
14Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni,
umekubali kuyapokea mkononi mwako.
Mhanga anajisalimisha kwako,
wewe ni msaada wa yatima.
15Vunja mkono wa mtu mwovu na mbaya,
mwite atoe hesabu ya maovu yake
ambayo yasingejulikana.
16BWANA ni Mfalme milele na milele,
mataifa wataangamia watoke nchini mwake.
17Unasikia, Ee BWANA, shauku ya wanaoonewa,
watie moyo nawe usikilize kilio chao,
18ukiwatetea yatima na walioonewa,
ili kwamba mwanadamu,
ambaye ni udongo,
asiogopeshe tena.
Copyright information for Neno