Psalms 109

Lalamiko La Mtu Aliyeko Kwenye Shida

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)

1Ee Mungu, ambaye ninakusifu,
usiwe kimya,
2kwa maana watu waovu na wadanganyifu
wamefungua vinywa vyao dhidi yangu;
wasema dhidi yangu
kwa ndimi za udanganyifu.
3Wamenizunguka kwa maneno ya chuki,
wananishambulia bila sababu.
4Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki,
lakini mimi ninawaombea.
5Wananilipiza baya kwa jema,
chuki badala ya urafiki wangu.
6Agiza mtu mwovu ampinge,
mshtaki
109.6 Mshtaki hapa maana yake ni Shetani
na asimame mkono wake wa kuume.
7Anapohukumiwa na apatikane na hatia,
nayo maombi yake na yamhukumu.
8Siku zake za kuishi na ziwe chache,
uongozi wake na apewe mtu mwingine.
9Watoto wake na waachwe yatima,
mke wake na awe mjane.
10Watoto wake na watangetange wakiomba-omba,
na wafukuzwe kwenye magofu
ya nyumba zao zilizobomoka.
11Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo,
matunda ya kazi yake
na yatekwe nyara na wageni.
12Asiwepo mtu ye yote wa kumtendea mema
wala wa kuwahurumia yatima wake.
13Uzao wake na ukatiliwe mbali,
majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho.
14Maovu ya baba zake na yakumbukwe
mbele za BWANA,
dhambi ya mama yake
na isifutwe kamwe.
15Dhambi zao na zibaki daima mbele za BWANA,
ili apate kukatilia mbali
kumbukumbu lao duniani.
16Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema,
bali alimfukuza mnyonge na mhitaji,
aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo.
17Alipenda kulaani,
nayo laana ikampata;
hakupenda kubariki,
kwa hiyo baraka na ikae mbali naye.
18Alivaa kulaani kama vazi lake,
nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji,
kwenye mifupa yake kama mafuta.
19Na iwe kama joho alilozungushiwa,
kama mshipi aliofungiwa daima.
20Haya na yawe malipo ya BWANA
kwa washtaki wangu,
kwa wale wanaoninenea mabaya.
21Lakini wewe, Ee BWANA Mwenyezi,
unitendee wema kwa ajili ya jina lako,
uniokoe kwa wema wako.
22Maana mimi ni maskini na mhitaji,
moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.
23Ninafifia kama kivuli cha jioni,
nimerushwa-rushwa kama nzige.
24Magoti yangu yamelegea kwa kufunga,
mwili wangu umedhoofika na kukonda.
25Nimekuwa kitu cha kudharauliwa
kwa washtaki wangu,
wanionapo, hutikisa vichwa vyao.
26Ee BWANA, Mungu wangu nisaidie,
niokoe sawasawa na upendo wako.
27Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako,
kwamba wewe, Ee BWANA,
umetenda hili.
28Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki,
watakaposhambulia wataaibishwa,
lakini mtumishi wako atashangilia.
29Washtaki wangu watavikwa fedheha,
na kufunikwa na aibu kama joho.
30Kwa kinywa changu nitamtukuza sana BWANA
katika umati mkubwa nitamsifu.
31Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji,
kuokoa maisha yake
kutoka kwa wale wanaomhukumu.
Copyright information for Neno