Psalms 115

Mungu Mmoja Wa Kweli

1Sio kwetu sisi, Ee BWANA, sio kwetu sisi
bali utukufu ni kwa jina lako,
kwa sababu ya upendo
na uaminifu wako.
2Kwa nini mataifa waseme,
“Yuko wapi Mungu wao?”
3Mungu wetu yuko mbinguni,
naye hufanya lo lote limpendezalo.
4Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
5Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
6zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
zina pua, lakini haziwezi kunusa;
7zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,
zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
8Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
9Ee nyumba ya Israeli, mtumainini BWANA,
yeye ni msaada na ngao yako.
10Ee nyumba ya Aroni, mtumainini BWANA,
yeye ni msaada na ngao yako.
11Ninyi mnaomcha, mtumainini BWANA,
yeye ni msaada na ngao yenu.
12BWANA anatukumbuka na atatubariki:
ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Aroni,
13atawabariki wale wanaomcha BWANA,
wadogo kwa wakubwa.
14BWANA na awawezeshe kuongezeka,
ninyi na watoto wenu.
15Mbarikiwe na BWANA
Muumba wa mbingu na dunia.
16Mbingu zilizo juu sana ni mali ya BWANA,
lakini dunia amempa mwanadamu.
17Sio wafu wanaomsifu BWANA,
wale washukao mahali pa kimya
115.17 Mahali pa kimya maana yake ni Kuzimu, yaani Sheol kwa Kiebrania
,
18bali ni sisi tunaomtukuza BWANA,
sasa na hata milele.
Msifuni BWANA
115.18 Msifuni BWANA ni Kiebrania Hallelu Yah
.
Copyright information for Neno