Psalms 116

Shukrani Kwa Kuokolewa Kutoka Mautini

Sifa Kwa Mungu

1Ninampenda BWANA kwa maana amesikia sauti yangu;
amesikia kilio changu ili anihurumie.
2Kwa sababu amenitegea sikio lake,
nitamwita siku zote za maisha yangu.
3Kamba za mauti zilinizunguka,
maumivu makuu ya kuzimu yalinipata,
nikalemewa na taabu na huzuni.
4Ndipo nikaliitia jina la BWANA:
“Ee BWANA, niokoe!”
5BWANA ni mwenye neema na haki,
Mungu wetu ni mwingi wa huruma.
6BWANA huwalinda wanyenyekevu,
nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa.
7Ee nafsi yangu, tulia tena,
kwa kuwa BWANA amekuwa mwema kwako.
8Kwa kuwa wewe, Ee BWANA,
umeniokoa nafsi yangu na mauti,
macho yangu kutokana na machozi,
miguu yangu kutokana na kujikwaa,
9ili niweze kutembea mbele za BWANA,
katika nchi ya walio hai.
10Niliamini, kwa hiyo nilisema,
“Mimi nimeteseka sana.”
11Katika taabu yangu nilisema,
“Wanadamu wote ni waongo.”
12Nimrudishie BWANA nini
kwa wema wake wote alionitendea?
13Nitakiinua kikombe cha wokovu
na kulitangaza jina la BWANA.
14Nitazitimiza nadhiri zangu kwa BWANA
mbele za watu wake wote.
15Kifo cha watakatifu kina thamani
machoni pa BWANA.
16Ee BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako,
mimi ni mtumishi wako,
mwana wa mjakazi wako
116.16 Au: mwanao mwaminifu
;
umeniweka huru
toka katika minyororo yangu.
17Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru
na kuliita jina la BWANA.
18Nitazitimiza nadhiri zangu kwa BWANA
mbele za watu wake wote,
19katika nyua za nyumba ya BWANA,
katikati yako, Ee Yerusalemu.
Msifuni BWANA.
Copyright information for Neno