Psalms 141

Maombi Ya Kuhifadhiwa Dhidi Ya Uovu

(Zaburi Ya Daudi)

1Ee BWANA, ninakuita wewe,
uje kwangu hima.
Sikia sauti yangu ninapokuita.
2Maombi yangu na yafike mbele zako
kama uvumba;
kuinua mikono yangu juu
na kuwe kama dhabihu ya jioni.
3Ee BWANA, weka mlinzi kinywani mwangu,
weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
4Usiuache moyo wangu uvutwe katika lililo baya,
nisije nikashiriki katika matendo maovu
pamoja na watu watendao mabaya,
wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
5Mtu mwenye haki na anipige:
ni jambo la huruma;
na anikemee,
ni mafuta kichwani mwangu.
Kichwa changu hakitalikataa.
Hata hivyo, maombi yangu daima
ni kinyume cha watenda mabaya,
6watawala wao watatupwa chini
kutoka kwenye majabali,
waovu watajifunza kwamba maneno yangu
yalikuwa kweli.
7Watasema, “Kama mtu anavyolima
na kuvunja ardhi,
ndivyo mifupa yetu imetawanywa
kwenye mlango wa kaburi.”
8Lakini nimekaza macho yangu kwako,
Ee BWANA Mwenyezi,
ndani yako nimekimbilia,
usiniache nife.
9Niepushe na mitego waliyonitegea,
kutokana na mitego
iliyotegwa na watenda mabaya.
10Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,
wakati mimi ninapita salama.
Copyright information for Neno