Psalms 143

Maombi Ya Kuokolewa Dhidi Ya Adui

(Zaburi Ya Daudi)

1Ee BWANA, sikia sala yangu,
sikiliza kilio changu unihurumie;
katika uaminifu na haki yako
njoo unisaidie.
2Usimhukumu mtumishi wako,
kwa kuwa hakuna mtu anayeishi
mwenye haki mbele zako.
3Adui hunifuatilia,
hunipondaponda chini;
hunifanya niishi gizani
kama wale waliokufa zamani.
4Kwa hiyo roho yangu inazimia ndani yangu,
moyo wangu ndani yangu unakata tamaa.
5Nakumbuka siku za zamani;
natafakari juu ya kazi zako zote,
naangalia juu ya kazi ambazo
mikono yako imezifanya.
6Nanyosha mikono yangu kwako,
nafsi yangu inakuonea kiu
kama ardhi kame.
7Ee BWANA, unijibu haraka,
roho yangu inazimia.
Usinifiche uso wako,
ama sivyo nitafanana
na wale washukao shimoni.
8Asubuhi uniletee neno la upendo wako usiokoma,
kwa kuwa nimeweka tumaini langu kwako.
Nionyeshe njia nitakayoiendea,
kwa kuwa kwako nainua nafsi yangu.
9Ee BWANA, uniokoe na adui zangu,
kwa kuwa nimejificha kwako.
10Nifundishe kufanya mapenzi yako,
kwa maana wewe ndiwe Mungu wangu,
Roho wako mwema na aniongoze
katika nchi tambarare.
11Ee BWANA, kwa ajili ya jina lako,
hifadhi maisha yangu,
kwa haki yako nitoe katika taabu.
12Kwa upendo wako usiokoma,
nyamazisha adui zangu;
waangamize watesi wangu wote,
kwa kuwa mimi ni mtumishi wako.
Copyright information for Neno