Psalms 144

Mfalme Amshukuru Mungu Kwa Ushindi

(Zaburi Ya Daudi)

1Sifa ni kwa BWANA Mwamba wangu,
aifundishaye mikono yangu vita,
vidole vyangu kupigana.
2Yeye ni Mungu wangu wa upendo na boma langu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
ngao yangu ninayemkimbilia,
ambaye huwatiisha mataifa chini yangu.
3Ee BWANA, mwanadamu ni nini hata umjali,
Binadamu ni nini hata umfikirie?
4Mwanadamu ni kama pumzi,
siku zake ni kama kivuli kinachopita.
5Ee BWANA, pasua mbingu zako, ushuke,
gusa milima ili itoe moshi.
6Peleka umeme wa radi na uwatawanye adui,
lenga mishale yako uwashinde.
7Nyosha mkono wako kutoka juu,
nikomboe na kuniokoa kutoka katika maji makuu,
kutoka katika mikono ya wageni
8ambao vinywa vyao vimejaa uongo,
mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
9Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
kwa zeze yenye nyuzi kumi nitakuimbia,
10kwa Mmoja awapaye wafalme ushindi,
ambaye humwokoa Daudi,
mtumishi wake na upanga hatari.
11Nikomboe na uniokoe
kutoka mikononi mwa wageni
ambao midomo yao imejaa uongo,
na mikono yao ya kuume ni midanganyifu.
12Kisha wana wetu wakati wa ujana wao
watakuwa kama mimea iliyotunzwa vizuri,
binti zetu watakuwa kama nguzo zilizoviringwa
kuremba jumba la kifalme.
13Ghala zetu zitajazwa
aina zote za mahitaji.
Kondoo zetu watazaa kwa maelfu,
kwa makumi ya maelfu
katika mashamba yetu;
14maksai wetu watakokota
mizigo mizito.
Hakutakuwa na kubomoka kuta,
hakuna kuchukuliwa mateka,
wala kilio cha taabu
katika barabara zetu.
15Heri watu ambao hili ni kweli;
heri wale ambao BWANA ni Mungu wao.
Copyright information for Neno