Psalms 16

Sala ya Matumaini

(Utenzi wa Daudi)

1Ee Mungu, uniweke salama,
kwa maana kwako nimekimbilia.
2Nilimwambia BWANA, “Wewe ndiwe Bwana wangu;
pasipo wewe sina jambo jema.”
3Kwa habari ya watakatifu walioko duniani,
ndio walio wa fahari ambao ninapendezwa nao.
4Huzuni itaongezeka kwa wale
wanaokimbilia miungu mingine.
Sitazimimina sadaka zao za damu
au kutaja majina yao midomoni mwangu.
5BWANA umeniwekea fungu langu na kikombe changu;
umeyafanya mambo yangu yote yawe salama.
6Alama za mipaka zimeniangukia mahali pazuri,
hakika nimepata urithi mzuri.
7Nitamsifu BWANA ambaye hunishauri,
hata wakati wa usiku moyo wangu hunifundisha.
8Nimemweka BWANA mbele yangu daima.
Kwa kuwa yupo mkono wangu wa kuume,
sitatikiswa.
9Kwa hiyo moyo wangu una furaha na ulimi wangu unashangilia;
pia mwili wangu utapumzika salama,
10kwa sababu hutanitelekeza kuzimu,
wala hutaacha Mtakatifu Wako aone uharibifu.
11Umenijulisha njia ya uzima;
utanijaza na shangwe katika uwepo wako,
pamoja na furaha za milele
katika mkono wako wa kuume.
Copyright information for Neno