Psalms 17

Sala Ya Mtu Asiye Na Hatia

(Sala Ya Daudi)

1Sikia, Ee BWANA, kusihi kwangu kwa haki,
sikiliza kilio changu.
Tega sikio kwa ombi langu,
halitoki kwenye midomo ya udanganyifu.
2Hukumu yangu na itoke kwako,
macho yako na yaone yale yaliyo haki.
3Ingawa unauchunguza moyo wangu
na kunikagua usiku,
ingawa umenijaribu,
hutaona cho chote,
nimeamua kwamba kinywa changu
hakitatenda dhambi.
4Kutokana na matendo ya wanadamu,
kwa neno la midomo yako,
nimejiepusha na njia
za wenye jeuri.
5Hatua zangu zimeshikamana na njia zako;
nyayo zangu hazikuteleza.
6Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu,
unitegee sikio lako na usikie ombi langu.
7Uonyeshe ajabu ya upendo wako mkuu,
wewe uokoaye kwa mkono wako wa kuume
wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.
8Nilinde kama mboni ya jicho lako,
unifiche chini ya kivuli cha mbawa zako
9kutokana na waovu wanaonishambulia,
kutokana na adui wauaji wanaonizunguka.
10Huifunga mioyo yao iliyo migumu,
vinywa vyao hunena kwa majivuno.
11Wamenifuatia nyayo zangu, sasa wamenizingira,
wakiwa macho, waniangushe chini.
12Wamefanana na simba mwenye njaa awindaye,
kama simba mkubwa anyemeleaye mafichoni.
13Inuka, Ee BWANA, pambana nao, uwaangushe,
niokoe kutokana na waovu kwa upanga wako.
14Ee BWANA, mkono wako uniokoe na watu wa jinsi hii,
kutokana na watu wa ulimwengu huu
ambao fungu lao liko katika maisha haya.
Na wapate adhabu ya kuwatosha.
Watoto wao na wapate zaidi ya hayo,
hukumu na iendelee kwa watoto wa watoto wao.
15Na mimi katika haki nitauona uso wako,
niamkapo, nitaridhika kwa kuona sura yako.
Copyright information for Neno