Psalms 30

Maombi Ya Shukrani

Utenzi Wa Kuweka Wakfu Hekalu (Zaburi Ya Daudi)

1Nitakutukuza wewe, Ee BWANA,
kwa kuwa umeniinua
na hukuacha adui zangu
washangilie juu yangu.
2Ee BWANA, Mungu wangu, nilikuita unisaidie
na wewe umeniponya.
3Ee BWANA, umenitoa Kuzimu,
umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
4Mwimbieni BWANA, enyi watakatifu wake;
lisifuni jina lake takatifu,
kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
5Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,
bali upendo wake hudumu siku zote;
inawezekana kilio kikawepo usiku kucha,
lakini asubuhi kukawa na furaha.
6Nilipofanikiwa nilisema,
“Sitatikiswa kamwe.”
7Ee BWANA, uliponijalia,
uliuimarisha mlima wangu,
lakini ulipouficha uso wako nilifadhaika.
8Kwako wewe, Ee BWANA, niliita,
kwa Bwana niliomba rehema:
9“Kuna faida gani katika kuangamia kwangu?
Katika kushuka kwangu shimoni?
Je, mavumbi yatakusifu?
Je, yatatangaza uaminifu wako?
10Ee BWANA, unisikie na kunihurumia,
Ee BWANA, uwe msaada wangu.”
11Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua nguo za gunia
ukanivika shangwe,
12ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.
Ee BWANA Mungu wangu,
nitakushukuru milele.
Copyright information for Neno