Psalms 31

Maombi na Sifa Kwa Kuokolewa Kutoka Kwa Adui

(Zaburi Ya Daudi)

1Ee BWANA, ninakukimbilia wewe,
usiache nikaaibika kamwe,
kwa haki yako uniokoe.
2Nitegee sikio lako, uje uniokoe haraka,
uwe kwangu mwamba wa kimbilio,
ngome imara ya kuniokoa.
3Kwa kuwa wewe ni mwamba wangu
na ngome yangu, uniongoze na kunilinda
kwa ajili ya jina lako.
4Uniepushe na mtego niliotegewa,
maana wewe ndiwe kimbilio langu.
5Ninaikabidhi roho yangu mikononi mwako,
Ee BWANA unikomboe,
wewe uliye Mungu wa kweli.
6Ninawachukia wale wanaong'ang'ania sanamu batili;
mimi ninamtumaini BWANA.
7Nitafurahia na kushangilia upendo wako,
kwa kuwa uliona mateso yangu
na ulijua maumivu ya nafsi yangu.
8Hukunikabidhi kwa adui yangu
bali umeiweka miguu yangu
mahali penye nafasi.
9Ee BWANA unihurumie, kwa kuwa niko kwenye shida;
macho yangu yanafifia kwa huzuni,
nafsi yangu na mwili wangu kwa sikitiko.
10Maisha yangu yamedhoofika kwa majonzi,
naam, miaka yangu kwa kulia kwa maumivu makali;
nguvu zangu zinaisha kwa ajili ya mateso,
na mifupa yangu inachakaa.
11Kwa sababu ya adui zangu wote,
nimedharauliwa kabisa na jirani zangu,
hata rafiki zangu wananiogopa,
wale wanionao barabarani hunikimbia.
12Nimesahaulika miongoni mwao kama mtu aliyekufa,
nimekuwa kama chombo cha mfinyanzi kilichovunjika.
13Kwa maana nimesikia maneno
niliyosingiziwa na watu wengi;
vitisho viko pande zote;
kwa kuwa wamefanya mashauri ya pamoja dhidi yangu
na kula njama kuniua.
14Lakini mimi ninakutumaini wewe peke yako, Ee BWANA;
nimesema, “Wewe ndiwe Mungu wangu.”
15Siku za maisha yangu ziko mikononi mwako,
uniokoe mikononi mwa adui zangu
na wale wanifuatiao.
16Mwangazie mtumishi wako uso wako,
uniokoe kwa ajili ya upendo wako usiokoma.
17Usiniache niaibike, Ee BWANA,
kwa maana nimekulilia wewe,
bali waovu waaibishwe
na kunyamazishwa Kuzimu.
18Midomo yao isemayo uongo na inyamazishwe,
kwa maana kwa kiburi na dharau husema
kwa majivuno dhidi ya wenye haki.
19Tazama jinsi ulivyo mkuu wema wako,
uliowawekea akiba wakuchao,
ambao huwapa wale wakukimbiliao
machoni pa watu.
20Unawahifadhi katika uvuli wa uwepo wako
kutokana na hila za wanadamu;
katika makao yako huwaweka salama
kutokana na ndimi za mashtaka.
21Atukuzwe BWANA,
kwa kuwa amenionyesha upendo wake wa ajabu
nilipokuwa katika mji uliozingirwa.
22Kwa haraka yangu nilisema,
“Nimekatiliwa mbali na macho yako!”
Hata hivyo ulisikia kilio changu
ukanihurumia nilipokuita unisaidie.
23Mpendeni BWANA ninyi watakatifu wake wote!
BWANA huwahifadhi waaminifu,
lakini wenye kiburi huwalipiza kikamilifu.
24Iweni hodari na mjipe moyo,
ninyi nyote mnaomtumaini BWANA.
Copyright information for Neno