Psalms 32

Furaha Ya Msamaha

(Utenzi: Zaburi Ya Daudi. Funzo)

1Heri mtu yule ambaye amesamehewa makosa yake,
ambaye dhambi zake zimefunikwa.
2Heri mtu yule ambaye BWANA
hamhesabii dhambi,
na ambaye rohoni mwake
hamna udanganyifu.
3Niliponyamaza, mifupa yangu ilichakaa
kwa kulia kwa maumivu makali
mchana kutwa.
4Usiku na mchana mkono wako ulinilemea,
nguvu zangu zilinyonywa
kama vile katika joto la kiangazi.
5Kisha nilikujulisha dhambi yangu
wala sikuficha uovu wangu.
Nikasema, “Nitaungama
makosa yangu kwa BWANA,”
ndipo uliponisamehe
hatia ya dhambi yangu.
6Kwa hiyo kila mtu mtauwa na akuombe
maadamu unapatikana,
hakika maji makuu yatakapofurika
hayatamfikia yeye.
7Wewe ndiwe mahali pangu pa kujificha,
utaniepusha na taabu
na kunizunguka kwa nyimbo za wokovu.
8Nitakufundisha na kukuonyesha
njia utakayoiendea;
nitakushauri na kukuangalia.
9Usiwe kama farasi au nyumbu
wasio na akili,
ambao ni lazima waongozwe
kwa lijamu na hatamu
la sivyo hawatakukaribia.
10Mtu mwovu ana taabu nyingi,
bali upendo usio na kikomo wa BWANA
unamzunguka mtu anayemtumaini.
11Shangilieni katika BWANA na mfurahi,
enyi wenye haki!
Imbeni, ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo!
Copyright information for Neno