Psalms 48

Sayuni, Mji Wa Mungu

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Wana Wa Kora)

1BWANA ni mkuu na anayestahili kusifiwa sana,
katika mji wa Mungu wetu,
mlima wake mtakatifu.
2Ni mzuri katika kuinuka kwake juu sana,
furaha ya dunia yote.
Kama vilele vya juu sana vya Safoni
48.2 Safoni inaweza ikawa na maana ya mlima mtakatifu au upande wa kaskazini
ni Mlima Sayuni,
mji wa Mfalme Mkuu.
3Mungu yuko katika ngome zake;
amejionyesha mwenyewe kuwa ngome yake.
4Wakati wafalme walipounganisha nguvu,
waliposonga mbele pamoja,
5walimwona nao wakashangaa,
wakakimbia kwa hofu.
6Kutetemeka kuliwashika huko,
maumivu kama ya mwanamke
mwenye utungu wa kuzaa.
7Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi
zilizovunjwa na upepo wa mashariki.
8Kama tulivyokuwa tumesikia,
ndivyo tulivyoona
katika mji wa BWANA Mwenye Nguvu Zote,
katika mji wa Mungu wetu:
Mungu ataufanya uwe salama milele.
9Ee Mungu, hekaluni mwako
tunatafakari upendo wako usiokoma.
10Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,
sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,
Mkono wako wa kuume umejazwa na haki.
11Mlima Sayuni unashangilia,
vijiji vya Yuda vinafurahi
kwa sababu ya hukumu zako.
12Tembeeni katika Sayuni,
uzungukeni mji,
hesabuni minara yake.
13Yatafakarini vyema maboma yake,
angalieni ngome zake,
ili mpate kusimulia habari zake
kwa kizazi kijacho.
14Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu
milele na milele;
atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.
Copyright information for Neno