Psalms 51

Kuomba Msamaha

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi Baada Ya Kukemewa Na Nabii Nathani Kwa Kuzini Na Bathsheba)

1Ee Mungu, unihurumie,
kwa kadiri ya upendo wako usiokoma,
kwa kadiri ya huruma yako kuu
uyafute makosa yangu.
2Unioshe na uovu wangu wote
na unitakase dhambi yangu.
3Kwa maana ninajua makosa yangu,
na dhambi yangu iko mbele yangu daima.
4Dhidi yako, wewe peke yako, nimetenda dhambi
na kufanya yaliyo mabaya machoni pako,
ili uthibitike kuwa mkweli unenapo
na kuwa na haki utoapo hukumu.
5Hakika mimi nilizaliwa mwenye dhambi,
mwenye dhambi tangu nilipotungwa mimba
kwa mama yangu.
6Hakika wewe wapendezwa na kweli itokayo moyoni,
ndani sana ya moyo wangu wanifundisha hekima.
7Unioshe kwa hisopo, nami nitakuwa safi,
unisafishe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.
8Unipe kusikia furaha na shangwe,
mifupa uliyoiponda na ifurahi.
9Uufiche uso wako usiitazame dhambi yangu
na uufute uovu wangu wote.
10Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
uifanye upya roho ya uthabiti ndani yangu.
11Usinitupe kutoka mbele zako
wala kuniondolea Roho wako Mtakatifu.
12Unirudishie tena furaha ya wokovu wako,
unipe roho ya utii, ili initegemeze.
13Ndipo nitakapowafundisha wakosaji njia zako,
na wenye dhambi watakugeukia wewe.
14Ee Mungu, Mungu uniokoaye,
niokoe na hatia ya kumwaga damu,
ulimi wangu utaimba juu ya haki yako.
15Ee BWANA, fungua midomo yangu,
na kinywa changu kitatangaza sifa zako.
16Wewe hupendezwi na dhabihu,
au ningaliileta,
hufurahii sadaka za kuteketezwa.
17Bali dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
moyo uliovunjika wenye toba,
Ee Mungu, hutaudharau.
18Kwa wema wa radhi yako uifanye Sayuni istawi,
ukazijenge upya kuta za Yerusalemu.
19Hapo ndipo kutakapokuwa na dhabihu za haki,
sadaka nzima za kuteketezwa
za kukupendeza sana,
pia mafahali watatolewa
madhabahuni mwako.
Copyright information for Neno