Psalms 94

Mungu Mlipiza Kisasi Kwa Ajili Ya Wenye Haki

1Ee BWANA, ulipizaye kisasi,
Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
2Ee mhukumu wa dunia, inuka,
uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
3Hata lini, waovu, Ee BWANA,
hata lini waovu watashangilia?
4Wanamimina maneno ya kiburi,
watenda mabaya wote wamejaa majivuno.
5Ee BWANA, wanawaponda watu wako,
wanawaonea urithi wako.
6Wanamchinja mjane na mgeni,
na kuwaua yatima.
7Nao husema, “BWANA haoni,
Mungu wa Yakobo hafahamu.”
8Sikia, enyi wajinga miongoni mwa watu,
enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
9Je, aliyeweka sikio asisikie?
Aliyeumba jicho asione?
10Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu?
Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
11BWANA anajua mawazo ya mwanadamu,
anajua ya kwamba hayafai.
12Ee BWANA, heri mtu anayeadhibishwa na wewe,
mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
13unampa utulivu siku za shida,
mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa
kwa ajili ya mwovu.
14Kwa kuwa BWANA hatawakataa watu wake,
hatauacha urithi wake.
15Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki,
wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
16Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu?
Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
17Kama BWANA asingelinisaidia upesi,
ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo.
18Niliposema, “Mguu wangu unateleza,”
Ee BWANA, upendo wako ulinishikilia.
19Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu,
faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
20Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe,
ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
21Huungana kuwashambulia wenye haki,
kuwahukumu kufa wasio na hatia.
22Lakini BWANA amekuwa ngome yangu,
na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
23Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao
na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao;
BWANA Mungu wetu atawaangamiza.
Copyright information for Neno