Psalms 101

Ahadi Ya Kuishi Kwa Uadilifu Na Kwa Haki

(Zaburi Ya Daudi)

Nitaimba juu ya upendo wako na haki yako;
kwako wewe, Ee BWANA,
nitaimba sifa.
Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama:
utakuja kwangu lini?
Nitatembea nyumbani mwangu
kwa moyo usio na lawama.
Sitaweka mbele ya macho yangu
kitu kiovu.
Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani;
hawatashikamana nami.
Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami;
nitajitenga na kila ubaya.
Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri,
huyo nitamnyamazisha;
mwenye macho ya dharau
na moyo wa kiburi sitamvumilia.
Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi,
ili waweze kuishi pamoja nami;
yeye ambaye moyo wake
hauna lawama atanitumikia.
Mdanganyifu hatakaa
nyumbani mwangu,
yeye asemaye kwa uongo
hatasimama mbele yangu.
Kila asubuhi nitawanyamazisha
waovu wote katika nchi;
nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya
kutoka katika mji wa BWANA.
Copyright information for Neno