Psalms 106

Wema Wa BWANA Kwa Watu Wake

Msifuni BWANA.
Mshukuruni BWANA, kwa kuwa ni mwema;
upendo wake wadumu milele.
Ni nani awezaye kusimulia
matendo makuu ya BWANA
au kutangaza kikamilifu sifa zake?
Heri wale wanaodumisha haki,
ambao daima wanafanya yaliyo mema.
Ee BWANA, unikumbuke unapowatendea mema watu wako,
uwe msaada wangu unapowaokoa,
ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako,
niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako,
na kuungana na urithi wako katika kukusifu.
Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda,
tumekosa na tumetenda kwa uovu.
Wakati baba zetu walipokuwa Misri,
hawakuzingatia maajabu yako,
wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako,
bali waliasi kando ya bahari,
Bahari ya Shamu.
Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake,
ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.
Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka,
akawaongoza katika vilindi vyake
kama vile jangwani.
10 Aliwaokoa kutoka mikononi mwa adui;
kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.
11 Maji yaliwafunika adui zao,
hakunusurika hata mmoja.
12 Ndipo walipoamini ahadi zake,
nao wakaimba sifa zake.
13 Lakini mara walisahau aliyowatendea,
wala hawakungojea shauri lake.
14 Jangwani walitawaliwa na tamaa zao,
walimjaribu Mungu nyikani.
15 Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba,
lakini akatuma juu yao
ugonjwa wa kudhoofisha.
16 Kambini waliwaonea wivu Mose na Aroni,
ambaye alikuwa amewekwa wakfu kwa BWANA.
17 Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani,
ikawazika Abiramu na kundi lake.
18 Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao,
mwali wa moto uliwateketeza waovu.
19 Huko Horebu walitengeneza ndama
na kuabudu sanamu ya kusubu
kutoka kwenye dhahabu.
20 Waliubadilisha Utukufu wa Mungu
na kuipa sanamu ya fahali,
ambaye hula majani.
21 Walimsahau Mungu aliyewaokoa,
ambaye alikuwa ametenda
mambo makuu huko Misri,
22 miujiza katika nchi ya Hamu
na mambo ya kutisha
huko Bahari ya Shamu.
23 Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza:
kama Mose mteule wake,
asingesimama kati yao na Mungu
kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.
24 Kisha waliidharau ile nchi nzuri,
hawakuiamini ahadi yake.
25 Walinung'unika ndani ya mahema yao,
wala hawakumtii BWANA.
26 Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa
kwamba atawafanya waanguke jangwani,
27 kuwatawanya wazao wao waanguke
miongoni mwa mataifa
na kuwatawanya katika nchi zote.
28 Walijifunga nira na Baali wa Peori,
wakala dhabihu zilizotolewa
kwa miungu isiyo na uhai,
29 waliichochea hasira ya BWANA,
wakamkasirisha kwa matendo yao maovu,
tauni ikazuka katikati yao.
30 Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati,
nayo tauni ikazuiliwa.
31 Hili likahesabiwa kwake haki,
kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.
32 Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha BWANA,
janga likampata Mose kwa sababu yao;
33 kwa maana walimwasi Roho wa Mungu
na maneno yakatoka midomoni kwa Mose bila kufikiri.
34 Hawakuyaangamiza yale mataifa
kama BWANA alivyowaagiza,
35 bali walijichanganya na mataifa
na wakazikubali desturi zao.
36 Waliabudu sanamu zao,
zikawa mtego kwao.
37 Wakawatoa wana wao
na binti zao dhabihu kwa mashetani.
38 Walimwaga damu isiyo na hatia,
damu za wana wao na binti zao,
ambao waliwatoa dhabihu
kwa sanamu za Kanaani,
nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.
39 Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda;
kwa matendo yao wenyewe
wakajifanyia ukahaba.
40 Kwa hiyo BWANA akawakasirikia watu wake
na akauchukia sana urithi wake.
41 Akawakabidhi kwa mataifa
na adui zao wakawatawala.
42 Adui zao wakawaonea
na kuwatia chini ya mamlaka yao.
43 Mara nyingi aliwaokoa
lakini wao walikuwa wamezama kwenye uasi,
nao wakajiharibu katika dhambi zao.
44 Lakini akaangalia mateso yao
wakati aliposikia kilio chao;
45 kwa ajili yao akakumbuka Agano lake
na kutokana na upendo wake mkuu
akapooza hasira yake.
46 Akawafanya wahurumiwe
na wote waliowashikilia mateka.
47 Ee BWANA Mungu wetu, utuokoe,
utukusanye tena kutoka kwa mataifa,
ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu
na kujisifu katika sifa zako.
48 Atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.
Watu wote na waseme, “Amen!”
Msifuni BWANA.
Copyright information for Neno