Psalms 108

Kuomba Msaada Dhidi Ya Adui

(Za 57:7-11; 60:5-12)

(Zaburi Ya Daudi. Wimbo)

Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti,
nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
Ee BWANA, nitakusifu katikati ya mataifa,
nitaimba sifa zako katikati ya mataifa.
Kwa maana upendo wako ni mkuu,
juu kuliko mbingu,
uaminifu wako hufika mpaka angani.
Ee Mungu, utukuzwe, juu ya mbingu,
utukufu wako na uwe duniani pote.
Utuokoe na kutusaidia kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
Mungu amesema kutoka patakatifu pake:
“Kwa furaha na ushindi nitaigawa Shekemu
na kulipima Bonde la Sukothi.
Gileadi ni yangu, Manase ni yangu,
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,
Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
Moabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
juu ya Ufilisti napiga kelele
ya furaha ya ushindi.”
10 Ni nani atakayenileta hadi kwenye mji wenye ngome?
Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
11 Si wewe, Ee Mungu, wewe ambaye umetukataa
nawe huendi tena na majeshi yetu?
12 Utusaidie kukabiliana na adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
13 Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,
naye atawaponda adui zetu.
Copyright information for Neno