Psalms 109

Lalamiko La Mtu Aliyeko Kwenye Shida

(Kwa Mwimbishaji: Zaburi Ya Daudi)

Ee Mungu, ambaye ninakusifu,
usiwe kimya,
kwa maana watu waovu na wadanganyifu
wamefungua vinywa vyao dhidi yangu;
wasema dhidi yangu
kwa ndimi za udanganyifu.
Wamenizunguka kwa maneno ya chuki,
wananishambulia bila sababu.
Wanachonilipa badala ya urafiki wangu ni kunishtaki,
lakini mimi ninawaombea.
Wananilipiza baya kwa jema,
chuki badala ya urafiki wangu.
Agiza mtu mwovu ampinge,
mshtaki
109.6 Mshtaki hapa maana yake ni Shetani
na asimame mkono wake wa kuume.
Anapohukumiwa na apatikane na hatia,
nayo maombi yake na yamhukumu.
Siku zake za kuishi na ziwe chache,
uongozi wake na apewe mtu mwingine.
Watoto wake na waachwe yatima,
mke wake na awe mjane.
10 Watoto wake na watangetange wakiomba-omba,
na wafukuzwe kwenye magofu
ya nyumba zao zilizobomoka.
11 Mtu anayemdai na ateke vyote alivyo navyo,
matunda ya kazi yake
na yatekwe nyara na wageni.
12 Asiwepo mtu ye yote wa kumtendea mema
wala wa kuwahurumia yatima wake.
13 Uzao wake na ukatiliwe mbali,
majina yao yafutike katika kizazi kifuatacho.
14 Maovu ya baba zake na yakumbukwe
mbele za BWANA,
dhambi ya mama yake
na isifutwe kamwe.
15 Dhambi zao na zibaki daima mbele za BWANA,
ili apate kukatilia mbali
kumbukumbu lao duniani.
16 Kwa maana kamwe hakuweza kutenda wema,
bali alimfukuza mnyonge na mhitaji,
aliwafanyia jeuri wahitaji na waliovunjika moyo.
17 Alipenda kulaani,
nayo laana ikampata;
hakupenda kubariki,
kwa hiyo baraka na ikae mbali naye.
18 Alivaa kulaani kama vazi lake,
nayo laana ikamwingia mwilini mwake kama maji,
kwenye mifupa yake kama mafuta.
19 Na iwe kama joho alilozungushiwa,
kama mshipi aliofungiwa daima.
20 Haya na yawe malipo ya BWANA
kwa washtaki wangu,
kwa wale wanaoninenea mabaya.
21 Lakini wewe, Ee BWANA Mwenyezi,
unitendee wema kwa ajili ya jina lako,
uniokoe kwa wema wako.
22 Maana mimi ni maskini na mhitaji,
moyo wangu umejeruhiwa ndani yangu.
23 Ninafifia kama kivuli cha jioni,
nimerushwa-rushwa kama nzige.
24 Magoti yangu yamelegea kwa kufunga,
mwili wangu umedhoofika na kukonda.
25 Nimekuwa kitu cha kudharauliwa
kwa washtaki wangu,
wanionapo, hutikisa vichwa vyao.
26 Ee BWANA, Mungu wangu nisaidie,
niokoe sawasawa na upendo wako.
27 Watu na wafahamu kuwa ni mkono wako,
kwamba wewe, Ee BWANA,
umetenda hili.
28 Wanaweza kulaani, lakini wewe utabariki,
watakaposhambulia wataaibishwa,
lakini mtumishi wako atashangilia.
29 Washtaki wangu watavikwa fedheha,
na kufunikwa na aibu kama joho.
30 Kwa kinywa changu nitamtukuza sana BWANA
katika umati mkubwa nitamsifu.
31 Kwa maana husimama mkono wa kuume wa mhitaji,
kuokoa maisha yake
kutoka kwa wale wanaomhukumu.
Copyright information for Neno