Psalms 113

Kumsifu BWANA Kwa Wema Wake

Msifuni BWANA.
Enyi watumishi wa BWANA msifuni,
lisifuni jina la BWANA.
Jina la BWANA na lisifiwe,
sasa na hata milele.
Kuanzia maawio ya jua hadi machweo yake,
jina la BWANA linapaswa kusifiwa.
BWANA ametukuka juu ya mataifa yote,
utukufu wake juu ya mbingu.
Ni nani aliye kama BWANA Mungu wetu,
Yeye ambaye ameketi juu
kwenye kiti cha enzi,
ambaye huinama atazame chini
aone mbingu na nchi?
Huwainua maskini kutoka mavumbini,
na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala,
huwaketisha pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake.
Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake,
akiwa mama wa watoto mwenye furaha.
Msifuni BWANA.
Copyright information for Neno