Psalms 118

Shukrani Kwa Ajili Ya Ushindi

1Mshukuruni BWANA, kwa kuwa ni mwema;
upendo wake wadumu milele.
2Israeli na aseme sasa:
“Upendo wake wadumu milele.”
3Nyumba ya Aroni na iseme sasa:
“Upendo wake wadumu milele.”
4Wote wamchao BWANA na waseme sasa:
“Upendo wake wadumu milele.”
5Wakati wa maumivu yangu makuu nilimlilia BWANA,
naye akanijibu kwa kuniweka huru.
6BWANA yuko pamoja nami, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
7BWANA yuko pamoja nami,
yeye ni msaidizi wangu.
Nitawatazama adui zangu kwa furaha
wakiwa wameshindwa.
8Ni bora kumkimbilia BWANA
kuliko kumtumainia mwanadamu.
9Ni bora kumkimbilia BWANA
kuliko kuwatumainia wakuu.
10Mataifa yote yalinizunguka,
lakini kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali.
11Walinizunguka pande zote,
lakini kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali.
12Walinizunguka kama kundi la nyuki,
lakini walikufa haraka kama miiba iteketeayo;
kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali.
13Nilisukumwa nyuma karibu kuanguka,
lakini BWANA alinisaidia.
14BWANA ni nguvu yangu na wimbo wangu,
yeye amefanyika wokovu wangu.
15Sauti za shangwe na ushindi
zinavuma hemani mwa wenye haki:
“Mkono wa kuume wa BWANA
umetenda mambo makuu!
16Mkono wa kuume wa BWANA
umeinuliwa juu,
mkono wa kuume wa BWANA
umetenda mambo makuu!”
17Sitakufa bali nitaishi,
nami nitatangaza yale BWANA aliyoyatenda.
18BWANA ameniadhibu vikali,
lakini hakuniacha nife.
19Nifungulie malango ya haki,
nami nitaingia na kumshukuru BWANA.
20Hili ni lango la BWANA
ambalo wenye haki wanaweza kuliingia.
21Nitakushukuru, kwa kuwa ulinijibu,
umekuwa wakovu wangu.
22Jiwe walilolikataa waashi,
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
23BWANA ametenda hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu.
24Hii ndiyo siku BWANA aliyoifanya,
tushangilie na kufurahi ndani yake.
25Ee BWANA, tuokoe,
Ee BWANA, utujalie mafanikio.
26Heri yule ajaye kwa jina la BWANA.
Kutoka katika nyumba ya BWANA tunakubariki.
27BWANA ndiye Mungu,
naye ametuangazia nuru yake.
Mkiwa na matawi mkononi,
unganeni kwenye maandamano ya sikukuu
hadi kwenye pembe za madhabahu.
28Wewe ni Mungu wangu, nitakushukuru,
wewe ni Mungu wangu, nitakutukuza.
29Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema;
upendo wake wadumu milele.
Copyright information for Neno